JULIAS MTATIRO AMPA SHULE WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA NA RAIS WAKE AWAAMBIE WASIUE DEMOKRASIA

TUSIUE DEMOKRASIA KWA KISINGIZIO CHA “HAPA KAZI TU”!
Na. Mtatiro J, “Darubini ya Mtatiro” Gazeti la Mwananchi, Jumapili 27 Disemba 2015
Tamko la Waziri Mkuu wa Jamhuri wa Tanzania mhe. Kasimu Majaliwa alilolitoa wilayani Ruangwa wakati anaongea na vyombo vya usalama wa ndani wa nchi kwamba, wagombea walioshindwa uchaguzi hawaruhusiwi kupita na kuwashukuru wananchi ni lazima ipingwe na kila mtu. Hii ni kauli hatari sana kutolewa na mtu wa hadhi ya Waziri Mkuu, ambaye hajamaliza hata mwezi mmoja madarakani.
Kauli hii ya Waziri Mkuu siyo yake peke yake, aliitoa kwa niaba ya serikali yake na kusisitiza kuwa “tumeshakubaliana ndani ya serikali”. Nimekosa maelezo mazuri ya kushangazwa na kauli hiyo lakini itoshe kusema kuwa mtu yeyote anayefuatilia siasa za Tanzania huku akijifunza kutoka katika siasa za nchi za wenzetu anajua kuwa hiyo ni kauli ya kupuuzwa na kudharauliwa kwa sababu inapingana na misingi ya kikatiba na kisheria ambayo nchi yetu imejiwekea.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzani imeshatoa haki mbalimbali na za msingi ambazo hata Rais hana uwezo wa kuzipokonya, ni haki za kikatiba.
Ibara ya 18.-(1) ya Katiba yetu inaeleza wazi kuwa “Bila ya kuathiri sheria za nchi, kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati”. Ibara hii inatoa uhuru kwa wananchi bila kujali vyeo wala kada, kutoa maoni na mawazo yao, kwenda mahali kwa ajili ya kupokea taarifa au kutoa taarifa, bila kujali mipaka ya nchi. Je Waziri Mkuu na serikali wameamua kukifuta kipengele hiki?
Ibara ya 18 (2) ya katiba ya Tanzania inaendelee kusisitiza kuwa “Kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi, na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii.” Waziri Mkuu na serikali wanapopiga marufuku wagombea walioshindwa katika uchaguzi kukutana na wananchi na kuongea nao kwa maana ya kuwashukuru, je wanatekeleza matakwa ya kikatiba ya ibara hii kutaka watu wapewe taarifa?
Ibara ya 20.-(1) ya katiba ya Tanzania imeeleza wazi kuwa “Kila mtu anastahili kuwa huru, bila ya kuathiri sheria za nchi, kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika na kushirikiana na watu wengine, kutoa mawazo hadharani, na hasa zaidi kuanzisha au kujiunga na vyama au mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi au kuendeleza imani au maslahi yake au maslahi mengineyo”. Ibara hii ina maana kwamba kila mtu bila kujali ni mgombea, alikuwa mgombea au hakuwa mgombea anayo haki ya kukutana na watu wengine bila kuathiri amani ya nchi? Hivi mgombea gani ambaye akienda kukutana na wananchi kwa hiyari (wananchi watakaotaka) atakuwa ameharibu au kuhatarisha amani na usalama wa nchi? Je, tamko la Waziri Mkuu na serikali limekanyaga kipengele hiki cha katiba kwa kiasi gani?
Ushahidi mwingine wa wazi uko kwenye Ibara ya 21.-(1) ya katiba ya Tanzania, inasomeka “Bila ya kuathiri masharti ya ibara ya 5, ya 39 na ya 67 ya Katiba hii na ya sheria za nchi kuhusiana na masharti ya kuchagua na kuchaguliwa, au kuteua na kuteuliwa kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi, kila raia wa Jamhuri ya Muungano anayo haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wa nchi, ama moja kwa moja au kwa kupitia wawakilishi waliochaguliwa na wananchi kwa hiari yao, kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa na sheria au kwa mujibu wa sheria”. Ibara hii inasisitiza kwamba kila mwananchi (mgombea, asiyekuwa mgombea, aliyeshinda uchaguzi, asiyeshinda uchaguzi n.k.) anayo haki ya kushiriki katika shughuli za utawala wan chi. Na ushiriki wa utawala wan chi unahusisha njia zote muhimu, kuwa mtendaji, kuwa mfuatiliaji na anayehoji ili serikali itende, kuchukua hatua za kushauri n.k. Najiuliza, kabla Majaliwa hajatoa tamko lile la “kidikteta” hakuwa amesoma katiba hii?
Huwenda tutamlaumu Waziri Mkuu wetu bure na serikali yake. Huwenda hakuwa ameisoma katiba ambayo aliahidi kuilinda, huwenda hajui alichokisema na madhara yake. Lakini kama ameshaikanyaga katiba, kwani hajui kuna sheria iliyoanzisha chama chake na ndiyo maana akawa mbunge kupitia chama hicho ambacho imefuzu vigezo vya kutoa Waziri Mkuu kwenye serikali ya sasa? Kasimu Majaliwa hajawahi kuisoma Sheria namba 258 ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002? (The Political Parties Act of 1992 as revised in 2002)?
Kifungu cha 11 cha sheria hii kimeeleza wazi kuwa kila chama cha siasa chenye usajili wa muda na wa kudumu kina haki zote za kufanya mikutano katika eneo lolote la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kutoa taarifa za mkutano huo kwa Ofisa wa Polisi anayehusika na eneo hilo. Kila chama cha siasa kinapaswa na kinabanwa na sheria kuvisaidia vyombo vya dola kutunza amani katika eneo hilo n.k. Mbona sheria ziko wazi kiasi hiki? Ni sheria ipi inayompa mamlaka Waziri Mkuu au serikali “ku-suspend” au kufuta haki za kikatiba na za kisheria za wananchi, vyama vya siasa n.k.?
Kama hakuna sheria inayompa mamlaka hayo Waziri Mkuu na serikali kutoa amri ya namna hii sisi wananchi ambao tunaamini kuwa Waziri Mkuu na serikali nzima waliapa kuilinda na kuitetea katiba ya Tanzania na sheria zake tueleweje? Je, Waziri Mkuu anatufundisha nini? Kwamba tuige nini kutoka kwake? Dharau kwa katiba! Kuipuuza sheria? Kwamba wananchi wa Tanzania wanapata mfano gani kutoka kwa kiongozi wao mkuu, anawafundisha wananchi wafanye nini? Yeye anafanya nini?
Matamko ya namna hii ya kimakusudi na yenye lengo la kujinufaisha kisiasa kwa chama kimoja ndiyo huwa yameleta vurugu na cmachafuko katika nchi nyingi za Afrika. Amani ya Tanzania haitalindwa kwa kuvunja katiba na kuondoa haki za kiraia, amani itadumu ikiwa haki za kiraia zinaheshimiwa na serikali. Amani itadumu ikiwa serikali na viongozi wake ndiyo wanakuwa mstari wa mbele katika kulinda na kutetea katiba ya Tanzania.
Majaliwa na serikali ya CCM wajitathmini upya, kauli mbiu ya hapa kazi tu ina maana ya kuhamasisha kila mtanzania achape kazi, kauli hiyo haina maana ya kuwapora watanzania haki zao za msingi.
Share on Google Plus

About KAKSIGABA

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment