Aliyekuwa
mgombea wa urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa amesema awamu ya
pili ya safari yake ya kuelekea Ikulu ndio kwanza imeanza na kuwataka
watu wote wanaomuunga mkono kutokata tamaa.
Lowassa,
ambaye ameshika nafasi ya pili katika mbio za urais wa Jamhuri ya
Muungano akiweka rekodi ya kukusanya kura milioni 6.07 ambayo ni rekodi
kwa mgombea wa upinzani, alitoa kauli hiyo jana mchana katika hafla ya
chakula cha mchana ya kuishukuru timu yake ya kampeni iliyofanyika Kawe,
Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi wakuu wa vyama vinavyounda
Ukawa, wanahabari na familia yake.
“Nimefarijika
sana, asanteni kwa msaada mlionipa, sina cha kuwalipa,” alisema waziri
huyo mkuu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne aliyeihama CCM na
kujiunga na Chadema mwezi Julai.
“Ukweli ni kwamba kila mmoja alifanya kazi yake. Tujiandae kwa awamu ya pili na safari ndiyo imeanza,” alisema na kushangiliwa.
“Unaweza kuchelewesha bahati ya mtu, lakini hauwezi kuiondoa,” aliongeza.
Hata hivyo, Lowassa hakueleza awamu ya pili itahusisha mambo gani.
Tangu
kumalizika kwa uchaguzi huo, Lowassa amezungumza na vyombo vya habari
mara mbili, mara ya mwisho akieleza jinsi alivyowasilisha pingamizi
lenye hoja tatu kuhusu mwenendo wa uchaguzi kwa mwenyekiti wa Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva ambalo liligonga mwamba.
Katika
tamko lake, Lowassa alikuwa akipinga matokeo ya kura za urais
yaliyokuwa yakitangazwa na NEC akidai kuwa si halisi na kuitaka isitishe
kutangaza, lakini tume hiyo haikueleza lolote na badala yake iliendelea
kutangaza matokeo ya majimbo na baadaye mshindi wa urais.
Mambo
hayo matatu yaliyowasilishwa NEC ni kupunguzwa kwa kura zake,
kuongezewa kura kwa mgombea wa CCM na kutangazwa matokeo batili kwa
wagombea wa Ukawa.
Lowassa
aliyeanza kwa kuwatambulisha watu wake wa karibu waliomshauri masuala
muhimu na nyeti katika kampeni, akiwemo waziri wa zamani wa Mambo ya
Ndani, Lawrence Masha, alizungumza kwa kifupi, akitoa mfano wa jinsi
majeshi ya ukombozi wa nchi mbalimbali barani Afrika yalivyorudi nyuma
kujipanga baada ya kushindwa.
Muda
mfupi kabla ya Lowassa kueleza hayo, mwenyekiti wa Chadema, Freeman
Mbowe aliufananisha Uchaguzi Mkuu na vita, akisema kulikuwa na njama za
makusudi za kuhakikisha Lowassa hapati ushindi.
Alisema
wagombea ubunge kutoka vyama vinavyounda Ukawa vya NCCR-Mageuzi,
Chadema, NLD na CUF, waliibiwa kura na ushindi kupewa wagombea wa CCM.
Mbowe alisema kwa kuwa hawawezi kupinga matokeo ya urais mahakamani, watafungua kesi za kupinga matokeo ya ubunge.
“Tunachofanya, tunarudi nyuma, tunajipanga kukata rufaa kupinga matokeo katika majimbo zaidi ya 30,” alisema Mbowe.
“Wagombea
wetu waliokuwa wabishi na kupigana kwelikweli walitangazwa washindi,
lakini kuna majimbo ambayo wagombea wetu waliporwa ushindi waziwazi
kabisa. Kwa kuwa ubunge unapingwa mahakamani tutafanya hivyo,” alisema
Mbowe.
Miongoni
mwa majimbo ambayo matokeo yake yalikuwa na ubishi ni Nyamagana, ambako
mbunge maarufu wa Chadema, Ezekiah Wenje alishindwa na mgombea wa
CCM,Stanslaus Mabula baada ya mvutano uliochukua muda mrefu. Pia mbunge
wa NCCR Mageuzi, David Kafulila wa Kigoma Kusini aliangushwa baada ya
matokeo kuibua mzozo mkali uliosababisha polisi kuingilia kati.
Mbowe
pia alisema kuwa wanahamishia nguvu Zanzibar kuungana na mgombea urais
kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Sharrif Hamad kudai haki yake.
Mbowe
alisema kitendo cha kufutwa kwa uchaguzi huo kina mkanganyiko mkubwa na
kusisitiza kuwa kuanzia wiki ijayo Ukawa itapiga kambi kwenye visiwa
hivyo kuhakikisha haki inatendeka.
Baadhi
ya viongozi wa Ukawa waliohudhuria hafla hiyo ni makamu mwenyekiti wa
Chadema –Bara, Profesa Abdallah Safari, mwenyekiti wa NCCR na mbunge
mteule wa Vunjo, James Mbatia na kaimu katibu Mkuu wa Chadema, Salum
Mwalimu.
-
Blogger Comment
-
Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments :
Post a Comment