
Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein (kushoto) na Makamu wake wa Kwanza, Maalim Seif Shariff Hamad
WANASIASA
wawili wanaogombania kutwaa urais katika uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa
Oktoba 25, walikutana mjini hapa jana na kuamsha upya “imani” miongoni
mwa wananchi kwa vile huo ni mkutano wa kwanza kwao tangu uchaguzi huo
ulipofutwa kinyemela Oktoba 28, mwaka huu.
Dk.
Ali Mohamed Shein aliyegombea tena urais kwa tiketi ya Chama Cha
Maponduzi (CCM), na Makamu wake wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Shariff
Hamad, aliyegombea kwa mara ya tano mfululizo, walikutana Ikulu ya
Zanzibar.
Hakuna
upande wowote kati ya viongozi hao uliotoa maelezo baada ya kukutana
kwao, ingawa vyanzo vya ndani ya serikali, Chama Cha Mapinduzi na Chama
cha Wananchi (CUF), vimethibitisha mazungumzo ya viongozi hao yalichukua
karibu saa nne kumalizika.
Mwandishi
wa habari hizi alipata taarifa awali kuwa ratiba ya kikoa cha viongozi
hao ilikuwa kuanzia saa 4 asubuhi hiyo jana, lakini inasemekana
kilichelewa kidogo kuanza. Lakini, hakuna sababu iliyoelezwa ya
ucheleweshaji huo na ni nani hasa alisababisha.
Katika
hatua nyingine, imeelezwa kwamba kikao cha viongozi hao, pia
kilimshirikisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali
Iddi, ambaye mwenyewe aligombea kiti cha uwakilishi, jimbo jipya la
Mahonda, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Taarifa
zaidi zimesema kwamba marais wawili wastaafu wa Zanzibar, Ali Hassan
Mwinyi aliyeongoza mwaka mmoja tu kufikia mwaka 1985 alipohamishiwa
Tanzania Bara na kuchaguliwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na
Amani Abeid Amani Karume, aliyeingia Ikulu Novemba 2000 na kutoka
Novemba 2010 baada ya kufanikisha mkataba wa kihistoria wa maridhiano na
Maalim Seif uliowezesha kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK)
baada ya uchaguzi mkuu.
Haifahamiki
ni katika mazingira gani aliitwa Mzee Mwinyi lakini akaachwa Dk. Salmin
Amour Juma ambaye aliongoza vipindi viwili kufikia 2000 ulipofanyika
uchaguzi mkuu.
Maofisa
wa Ikulu ya Zanzibar hawakuwa tayari kueleza undani wa kikao cha
viongozi hao, lakini wale wa CUF walithibitisha kuwa majadiliano
yalikuwa “ni mema kwa maslahi ya nchi.”
Zipo
taarifa kwamba ni Maalim Seif aliyetaka Mzee Mwinyi ashiriki kikao
hicho, lakini hakuna aliyethibitisha taarifa hizo, na wala haikuelezwa
sababu ya kualikwa kiongozi mstaafu huyo ambaye kwa Wazanzibari wapenda
mabadiliko, anaonekana kama “adui” wa maendeleo ya Zanzibar.
Tangu
kustaafu uongozi mwaka 2000, Dk. Salmin amekuwa haonekani mara kwa mara
hadharani kutokana na hali yake ya afya. Hata kabla ya kustaafu,
alipata upofu wa macho, na mara ya mwisho alipokutana na waandishi wa
habari nyumbani kwake Migombani, mjini haopa, alisema, “sasa hivi
angalau naweza kusoma magazeti, sijambo alhamdulillahi.”
Hata hivyo, hali yake ilionekana wazi kuwa macho yake hayakuwa na uwezo tena wa kusoma chochote, na kwa jumla kuona.
Ingawa
hakuna maelezo ya undani wa mazungumzo yalivyokuwa, kule kukutana kwa
Dk. Shein na Maalim Seif wakati huu, kunaweza kurudisha imani kwamba
utatuzi wa mgogoro uko nchani kupatikana.
Kikao
kilichowakutanisha Dk. Shein na makamu wake wawili kimefanyika ndani ya
hali isiyoeleweka kwa sasa, kwa vile nchi imeganda baada ya kuingizwa
kwenye mgogoro wa uchaguzi mkuu.
Mgogoro
huo umetokana na hatua ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar
(ZEC), Jecha Salim Jecha, kutangaza uamuzi wa “peke yake” wa kufuta
uchaguzi wote nchi nzima huku akiwa ameshatangaza matokeo ya urais kwa
majimbo 31 kati ya 54 yote ya Zanzibar.
Uamuzi
huo unatambuliwa kuwa ni wa peke yake, kwa sababu umethibitishwa
kutokana na majadiliano ya ndani ya Tume hiyo, na kwa kuwa si yeye
mwenyekiti wala Tume, yenye mamlaka ya kisheria ya kufanya hivyo.
Hakuna
kifungu cha sheria katika Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar, Na. 11 ya
mwaka 1984, wala katika Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984, kinachotoa
mamlaka hayo kwa namna yoyote ile.
Hii
imethibitishwa na tamko lake mwenyewe Jecha ambalo pamoja na kuwa
alilisaini, hakueleza amepewa mamlaka hayo na kifungu gani cha sheria.
Jecha
alitangaza uamuzi huo Oktoba 28, siku ya pili, makamishna wawili wa
Tume hiyo kutoka CUF, Nassor Khamis Mohamed, na Ayub Bakari, walimkana
wakieleza kuwa alichokifanya si halali kwani hakuna mamlaka yaliyompa
nguvu, na hakuna kikao cha Tume kilichofanyika hata kufikia uamuzi wa
kumtuma kufanya hivyo.
Aidha,
Jecha alitoa tangazo hilo siku mbili baada ya Maalim Seif kueleza
kwamba mwelekeo wa kura ulikuwa wa kumpatia ushindi wa asilimia 52.87
dhidi ya asilimia 47.13 za Dk. Shein.
Maalim
Seif aliyetoa taarifa hiyo mbele ya waandishi wa habari, kwenye makao
makuu ya CUF, alisema alitarajia Tume itangaze matokeo pasina
kuchelewesha na kumtaka Dk. Shein akubali amepoteza mamlaka na kutangaza
rasmi kama alivyofanya yeye mwaka 2010.
Kukutana
kwa viongozi hao kunachukuliwa kama hatua muhimu katika kurudisha
“wanasiasa wahafidhina wa CCM” katika ufahamu wao wa akili kwa vile
dunia inauhakika kuwa wao ndio tatizo.
Matokeo
ya uchaguzi yalikuwa tayari yamesainiwa na wasimamizi wa vituo vya
uchaguzi nchi nzima katika majimbo yote 54, na hata wakala mkuu wa Dk.
Shein, Balozi Mohamed Ramiya Abdiwawa, alisharidhia na ikaelezwa
“aliharakia kumpa taarifa ya kushindwa Dk. Shein.”
“Ukweli
Dk. Shein ameingizwa tu katika mgogoro ili aonekane tatizo, lakini
aliharakia kukubali kushindwa na kusema, ‘siwezi kubadilisha uamuzi wa
wananchi.”
Viongozi
wanaotajwa kuchimba mgogoro ni wale watatu walioonekana kwenye vyombo
vya habari Oktoba 29, wakitoa malalamiko kuwa CCM ilihujumiwa.
Hao
ni Spika Pandu Ameir Kificho,Waziri Kiongozi mstaafu Shamsi Vuai
Nahodha na Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Vuai Ali Vuai ambao duru ndani ya
CCM zinasema wanaungwa mkono na Balozi Seif.
0 comments :
Post a Comment