TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
KAULI YA MWENYEKITI FREEMAN MBOWE
KUHUSU
UAMUZI WA BODI YA MCC KUZUIA MSAADA WAKE KWA SERIKALI YA TANZANIA
Muda mfupi baada ya Bodi ya MCC kutoa taarifa inayoonesha Tanzania
haitapata msaada kutoka shirika hilo kama ilivyotarajiwa kwa ajili ya
mwaka 2016, Mwenyekiti wa Chama (T), Freema Mbowe ametoa kauli nzito juu
ya suala hilo akisema kuwa kuchelewa kupatikana kwa fedha za MCC si tu
kunachafua jina la nchi na hadhi yake katika medani za kimataifa, bali
kutaathiri kwa kiasi kikubwa miradi yote iliyo chini ya ufadhili wa MCC.
MCC imeahirisha msada huo wa USD Mil. 472.8 ambazo ni takriban trilioni
moja kwa fedha za Tanzania zilizolengwa kusaidia sekta ya nishati ya
umeme hususan ule wa vijijini, katika kuunganisha wateja wapya,
mabadiliko ya kimuundo ya Shirika la Umeme nchini (TANESCO) ili lifanye
kazi na kutoa huduma kwa ufanisi katika sehemu za uzalishaji,
usafirishaji na usambazaji.
Fedha hizo pia zilikusudiwa kusaidia kuanza kwa mpango mkubwa wa kuboresha sekta ya umeme nchini.2014-2024.
Mbowe amemtaka Rais John Magufuli kuchukua hatua za haraka za kiuongozi
kumaliza mtanziko wa kisiasa Zanzibar kwa mshindi wa nafasi ya urais
kutangazwa kutokana na uchaguzi uliofanyika mwezi Oktoba, mwaka huu.
Aidha amesema kuwa Sheria ya makosa ya mtandao (Cyber Crime Act 2015)
ambayo ni mojawapo ya sababu zilizotumiwa na MCC kuahirisha msaada huo
kwa Tanzania hadi itakapokuwa imefanyiwa kazi, ni sheria mbaya sana
inayokinzana na kukua kwa technologia ya habari na mawasiliano na kuzuia
upashanaji wa habari miongoni mwa jamii ambayo ililenga kuweka makosa
ya kijinai ili kudhibiti wapinzani wa CCM katika uchaguzi mkuu na
kukipatia mazingira ya ushindi chama hicho.
"Sasa imethibitika
kuwa Bodi ya MCC iliyokaa tarehe 16 Dec 2015 imeahirisha rasmi
kuidhinisha msaada wa Millenium Challenge uliokuwa umekusudiwa kwa
Tanzania kwa mwaka wa fedha 2016. Sababu kuu mbili zilizosababisha
uamuzi huo ni:
1. Mkwamo wa Uchaguzi wa Rais na Wawakilishi Zanzibar na
2.Matumizi mabaya ya she ria ya makosa ya mtandao hususan kuhusiana na
uchaguzi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa 2015."
"Ubabe
wa baadhi ya viongozi wa CCM ni janga la Taifa. Kuchelewa kupatikana
kwa fedha za MCC si tu kunachafua jina la nchi na hadhi yake katika
medani za kimataifa, bali kutaathiri kwa kiasi kikubwa miradi yote iliyo
chini ya ufadhili wa MCC," amesema Mwenyekiti Mbowe na kuongeza;
"Sheria ya makosa ya mtandao (Cyber Crime Act 2015) ni sheria mbaya
sana inayokinzana na kukua kwa technologia ya habari na mawasiliano.
Aidha, kwa makusudi kabisa inafifisha uhuru wa kupashana habari na ni
dhahiri ilitungwa kwa nia mbaya ya kuthibiti kijinai uchaguzi mkuu."
"Tuliipinga sheria hii Bungeni na ikapitishwa usiku wa manane kwa ubabe
wa wabunge wa CCM na hata tulipomtaka rais Kikwete asiisaini aliisaini
kibabe akijua anaandaa mazingira gani ya "kihalifu", " amesema
Mwenyekiti Mbowe.
Ameongeza kusema kuwa sheria hiyo ilitumika
kuvamia vituo vya CHADEMA vilivyokuwa vikitumika kukusanya matokeo ya
kura za rais na wabunge na hadi leo vijana zaidi ya 161, wakiwemo
wanafunzi, wana kesi za "kubumba" mahakamani.
Mwenyekiti Mbowe
amesema kuwa Sheria hiyo hiyo ilitumika kuficha dhana ovu iliyotumika
kuhalalisha kuvamia Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC)
kilichokuwa kikiratibu watazamaji wa uchaguzi wa ndani kwa kibali cha
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
"Vile vile Sheria hii imetumika
kuwakamata na kuwaweka ndani na hata kuwanyima dhamana vijana wetu ambao
walituunga mkono katika uchaguzi mkuu."
"Namtaka rais Magufuli achukue hatua za kiuongozi na kiutawala kwa kufanya yafuatayo:"
"Kwanza aumalize mgogoro wa kisiasa Zanzibar kwa kuhakikisha kuwa mshindi halali anatangazwa.
"Pili achukue hatua ya kuifanyia marekebisho makubwa Sheria ya makosa
ya mtandao katika bunge lijalo. Aidha wale wote waliobambikiwa kesi
amuamuru DPP kuzifuta kesi hizo mara moja," amesema.
Mwenyekiti
Mbowe amesisitiza kuwa Rais Magufuli hana budi kuchukua hatua hizo za
haraka ili kulinusuru taifa na hasara ya kupoteza mabilioni hayo ya MCC
na zaidi kuepusha kuporomoka zaidi kwa biashara ya utalii nchini
Zanzibar.
Amesema katika taifa ambalo sekta ya umeme inakabiliwa
na matatizo makubwa katika uzalishaji, usambazaji na usafirishaji huku
wananchi wa kipato cha chini wakibebeshwa mzigo mkubwa wa kumudu nishati
hiyo na wengine wakilazimika kutumia nishati mbadala kama mkaa
unaotokana na miti hivyo kusababisha uharibifu wa mazingira, serikali
inayojua wajibu wake yenye viongozi wanaothamini uwajibikaji, haikupaswa
kushindwa kuchukua hatua stahiki kutimiza vigezo vya msaada huo ambao
umeshaisaidia Tanzania katika miradi mingine kadhaa.
Imetolewa leo Ijumaa, Desemba 18, 2015 na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA
-
Blogger Comment
-
Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments :
Post a Comment