JESHI
la Polisi Nchini lipo mbioni kumkamata Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman
Mbowe kwa kudaiwa kutorosha mabilioni ya fedha kwenda nchi mbalimbali za
Bara za Asia.
Uchunguzi uliofanywa na JAMVI LA HABARI, umebaini kwa kiasi kikubwa
uchunguzi uliokuwa unafanywa na Kitengo cha Uchunguzi wa Fedha kilicho
chini ya Wizara ya Fedha (FIU) kimekamilika huku Polisi ikitarajia
kuanza kuchukua hatua zaidi.
Taarifa ilizozipata gazeti hilo kutoka FIU, ilisema tayari kila kitu
kimemalizika na kilichobaki ni suala hilo, kulipeleka Polisi kwa ajili
ya kuchukua uamuzi zaidi wa jambo hilo.
"Tumemaliza kila kitu na kilichobaki ni Polisi, lakini mie sio msemaji
wa suala hilo, ungezungumza na watu wa FRAUD kutoka Polisi, ambao
watakupa nafasi nzuri ya suala hilo, ambalo ni kubwa sana,''alisema.
Hata hivyo, Gazeti hili liliwasiliana na mmoja wa askari wanaoelezwa
kulishikiria suala hilo, Salum Kisai, ambapo alisema yeye sio msemaji na
kumtaka mwandishi awasiliane na Kamanda wa Upelelezi wa Kanda Maalumu
ya Dar es Salaam, ZCO Costastine Massawe na kukata simu.
"Embu wasiliana na ZCO mie sio msemaji wa suala hilo,''alisema na kukata simu.
Mbowe, ambaye alisafirisha fedha hizo mwanzoni mwa mwezi wa Agosti,
mwaka huu baada ya kuamisho mabilioni ya fedha kwenye akaunti yake hivi
karibuni bila kuwa na vielelezo vya kufanya hivyo na kutakiwa kukamatwa
na kumfikisha katika vyombo vya dola.
Mbowe, ambaye pia ni Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Mbunge wa Hai na
mfanyabiashara mwenye makampuni mengi hapa nchini, amefanya uhamisho huo
wa fedha kwa kutumia kampuni isiyofahamika sana ijulikanayo kwa jina la
Aretra World Wide Limited na imethibitika kwamba amefanya uhamisho huo
wa fedha kwa kumtumia mtu anayeitwa Junaid Ali, ambaye ni Meneja wa
Mahusiano ya Wateja wa Benki ya Noor ya Falme za Kiarabu mwezi huo.
Taarifa zaidi zinathibitisha kwamba, Kwa kumtumia Ali, Mbowe aliagiza
fedha hizo zipelekwe katika akaunti tatu tofauti ambazo zote ziko nje ya
Tanzania.
Kampuni hizo na kiasi cha fedha kilichopelekwa ni Puku Hong Kong Limited
iliyotumiwa dola 230,555 (shilingi milioni 461), TanChin Trading Co.
Limited iliyotumiwa dola 302,614 (shilingi milioni 605) na Hong Kong Da
Web International Tradings Limited iliyotumiwa dola 489,860 (shilingi
milioni 980). Jumla ya fedha zote zilizohamishwa ni zaidi ya shilingi
bilioni mbili.
Makampuni yote yaliyotumiwa fedha yana ofisi zake nchini Hong Kong na yote yamefunguliwa akaunti katika benki maarufu ya HSBC.
Junaid Ali ambaye amepewa maelekezo ya kufanya malipo hayo ni mtaalamu
wa masuala ya kufungua makampuni yanayojulikana kama offshore ambayo
mara nyingi hutumiwa na wafanyabiashara kufanya malipo pasipo kujulikana
na watu.
Taarifa zinaendelea kusema kwamba makampuni ya namna hii hufunguliwa
katika nchi zenye usiri mkubwa kwa watu wanaohifadhi fedha na ndiyo
maana wakati wa sakata la ununuzi wa rada, Andrew Chenge na aliyekuwa
Gavana wa Benki Kuu (BoT), Dk. Idris Rashid, walitumiana fedha kupitia
akaunti zao zilizo katika nchi zinazoongoza kwa kuwa na makampuni mengi
ya namna hii.
Akimwandikia Junaid, Freeman Mbowe alisema; "Tafadhali, nakuomba na kwa
haraka, ufanye uhamishaji wa fedha kutoka katika benki yako na kwenda
kwenye akaunti zifuatazo; Puku, TanChin na Hong Kong Da Web," aliandika
Mbowe.
Katika barua hiyo ambayo JAMVI LA HABARI imefanikiwa kuona nakala yake,
Mbowe ameitambulisha kampuni yake kwa anuani ya S.LP 293816, iliyopo
katika jengo la World Trade Centre, Mtaa wa Sheikh Zayed, Dubai falme
za kiarabu.
Kwa kuwa kampuni hiyo ya Mbowe ni offshore, gazeti hili limeshindwa
kufahamu ni kiasi gani cha fedha Mbowe amehifadhi au ameweka kwenye
akaunti hiyo na chanzo cha mapato hayo ni kipi kwa vile biashara zake
nyingi anafanya hapa nchini, ingawa ameanza kujitanua kimataifa.
Sambamba na hilo , uchunguzi wa gazeti hili umebaini kwamba Mbowe
alitakiwa kupokea kiasi cha dola 330,000 (shilingi milioni 660)
takribani sawa na fedha aliyoihamishia TanChin Hong Hong, kutoka kwa
wafadhili wa chama hicho waliopo nchini Japan.
Kwa mujibu wa mawasiliano baina ya viongozi wa juu wa Chadema na
wafadhili hao wa kijapani kupitia kwa mtu anayefahamika kwa jina la
Naomi pamoja na Mchungaji Mariko Morikubo, Chadema ilikuwa ichangiwe
fedha za kijapani (Yen), milioni 40 ambazo ni sawa na dola 330,000 kabla
ya mwisho wa Julai mwaka huu.
Ndani ya CHADEMA, ni viongozi wakuu watatu ndiyo wanaonekana kushiriki
katika mazungumzo hayo; Mbowe, Slaa na Reginald Munisi ambaye ni
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa chama hicho.
Mpaka sasa haijafahamika mara moja ni kwa nini Mbowe amehamisha kiasi
kikubwa namna hiyo cha fedha na kukipeleka nje ya nchi na kwamba
imeendelea kutia mashaka kama kuna kodi halali ya serikali imekatwa
katika muamala huo.
Wakizungumza na gazeti hili lilipotaka kujua mtazamo wao kuhusu
kinachoitwa 'utumbuaji majipu wa Magufuli' wananchi kadhaa wamesema
hicho nacho ni moja kati ya kipimo kikubwa cha uimara wa serikali ya
Magufuli na kwamba kama ataweza kumkamata Mbowe basi ataonekana kweli
amedhamiri kulikomboa taifa letu na kuthibitisha msemo kwamba sheria ni
msumeno.
Abdallah Hussein, mkazi wa Kichangani Morogoro amesema, ili nchi yoyote
inayofuata na kuheshimu utawala wa sheria ni lazima watu wote waishi
misingi na utaratibu wa nchi hiyo, Hussein amesisitiza ikiwa Mbowe
ameweza kufanya hivyo na kama hatua haitachukuliwa dhidi yake, basi kuna
uwezekano mkubwa wa wanasiasa wengine kutumia uanasiasa wao kufanya
biashara halali na haramu kujinufaisha.
"Hebu ona hii,mtu kama mbowe anaweza kusafirisha zaidi ya bilioni mbili
kiharaka haraka hivyo, unatarajia kuna uhalali hapo? ,nani amekagua
hizo hela na kuthibitisha ni halali na hazina madhara wala viashiria vya
rushwa?"
Ameendelea kushangaa na kuonyesha taadhari ya hali ya juu na kumtaka
Rais Magufuli kuhakikisha anaendelea kutumbua majipu na kusisitiza
kwamba asimuangalie mtu yeyote usoni na kwamba ni lazima sasa vyombo vya
dola vikachukua nafasi yake na kuthibitisha uhalali wa fedha hizo .
Taarifa ambazo gazeti hili linazo zinasema kwamba kitengo cha udhibiti
wa Fedha FIU kinaendelea kulishuhulikia suala hilo na kwamba inatarajiwa
hatua kuchukuliwa wakatio wowote kutoka sasa.
Mara kadhaa Mbowe amekaririwa kama mtu anayetetea sana uwepo wa utawala
wa sheria na kwamba amekuwa akiilaumu serikali na taasisi nyingine
zisipofuata sheria, jambo ambalo yeye pia anakabiliwa nalo hivi sasa,.
Ikiwa FIU watakamilisha uchunguzi wao haraka kama inavyotarajiwa, jeshi
la polisi litakuwa na wajibu wa kumkamata na kumfikisha mahakamani kwa
tuhuma za usafirishaji fedha isivyo halali.
Chanzo: Gazeti la JAMVI LA HABARI
-
Blogger Comment
-
Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments :
Post a Comment