Serikali Imetoa Waraka wa ElimuBure......Shule 11 za Serikali Hazitahusika na Utoaji wa Elimu Bure
WIZARA ya Elimu, Sayansi na Ufundi imetoa waraka wa elimu kuhusu
elimumsingi bila malipo na kutoa orodha ya shule za msingi 11 za
Serikali ambazo hazihusiki na utoaji wa elimu bure uliotangazwa na Rais
John Magufuli.
Elimumsingi inajumuisha elimu ya awali, ya msingi na sekondari ambayo itaanza Januari mwakani.
Katika Waraka Elimu Namba 6 wa Mwaka 2015 kuhusu utekelezaji wa elimu
bure kwa shule za msingi na sekondari, wizara hiyo imetaja shule hizo
kuwa ni Shule ya Msingi Olympio (Dar es Salaam); Shule ya Msingi Diamond
(Dar es Salaam); Shule ya Msingi Oysterbay (Dar es Salaam); Shule ya
Msingi Iringa (Iringa) na Shule ya Msingi Mkapa (Mbeya).
Nyingine
ni Shule ya Msingi Angaza (Mbeya); Shule ya Msingi Nuru (Mbeya); Shule
ya Msingi Lupilisi (Ruvuma); Shule ya Msingi Tanga (Tanga); Shule ya
Msingi Arusha (Arusha) na Shule ya Msingi Kisimani iliyoko mkoani
Arusha.
Wizara hiyo pia imesema waraka huo hauzihusu shule
zinazomilikiwa na mashirika ya umma ama taasisi za umma ambazo
zinaendeshwa kwa taratibu sawa na shule za binafsi.
Katika
waraka huo, wizara hiyo imetoa majukumu yanayotakiwa kufanywa na Wizara
hiyo, Tamisemi, wakurugenzi wa manispaa na halmashauri ya wilaya, wakuu
wa shule, bodi za shule, wazazi na wananchi.
Majukumu ya wazazi na walezi
Kuanzia Januari, wazazi wanatakiwa tu kununua sare za shule na michezo,
vifaa vya kujifunzia vikiwemo madaftari na kalamu, na chakula kwa
wanafunzi wa kutwa na kugharimia matibabu kwa watoto wao.
Wanatakiwa pia kulipia nauli ya kwenda shule na kurudi kwa wanafunzi wa
kutwa na wanafunzi wa bweni wakati wa likizo; kununua magodoro, shuka,
vifaa vya usafi binafsi kwa wanafunzi wanaosoma shule za bweni na
wanaoishi katika hosteli zinazotumiwa na serikali; na kukemea na kutoa
taarifa kuhusu mienendo inayokwenda kinyume na elimumsingi bila malipo.
Wazazi na wananchi wengine pia wanatakiwa kuendelea kujitolea nguvukazi
na mali ili kuleta ustawi na maendeleo ya shule zilizoko ndani ya
jamii.
Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi
Katika
waraka huo, Wizara ina jukumu la kutenga fedha za kugharimia
utayarishaji na uendeshaji wa mitihani ya kitaifa kulingana na idadi ya
wanafunzi; kutenga fedha kwa ajili ya Uthibiti Ubora wa Shule na kutenga
fedha za kufanya ufuatiliaji na tathmini ya utoaji wa elimumsingi bila
malipo na kuchukua hatua stahiki pale inapobidi.
Inachotakiwa
kufanya Tamisemi Kwa upande wa Tamisemi, waraka huo unaielekeza wizara
hiyo kutoa miongozo ya matumizi ya fedha za umma kwa wakuu wa shule,
kuratibu uandaaji wa mipango na bajeti ili kupata mipango na bajeti ya
taifa kila mwaka inayozingatia mahitaji halisi ya elimumsingi bila
malipo.
Pia Tamisemi inatakiwa kufanya ukaguzi wa ndani,
ufuatiliaji na tathmini za mara kwa mara ili kuhakikisha elimumsingi
bila malipo inatolewa kwa ufanisi na viwango vya ubora inavyostahili.
Kuratibu utoaji mipango na bajeti za ruzuku ya uendeshaji wa shule
ikiwemo ulinzi, umeme, maji na ununuzi wa chaki na karatasi pamoja na
vifaa vingine vya kufundishia na kujifunzia.
Kutenga na kutuma
fedha shuleni kwa ajili ya uendeshaji na usimamizi wa mitihani na
majaribio mbalimbali shuleni ikiwemo tathmini endelezi, kununua vitabu,
kemikali na vifaa vya maabara, samani yakiwemo madawati, vifaa vya
michezo, matengenezo ya mashine na mitambo pamoja na kujenga na
kukarabati miundombinu ya shule.
Kutenga na kutuma fedha shuleni
za kugharimia wanafunzi wenye mahitaji maalumu waliopo kwenye shule na
vitengo vya elimu maalumu kwa kuwapatia chakula yaani mlo mmoja kwa
wanafunzi wa kutwa na milo mitatu kwa wanafunzi wa bweni pamoja na vifaa
na visaidizi.
Wakuu wa shule
Waraka huo unawataka wakuu wa
shule kuwapa maelekezo wazazi kuhusu aina ya vifaa vinavyohitajika mfano
rangi ya kitambaa cha sare ya shule, sare za michezo, idadi na aina ya
madaftari watakayotumia wanafunzi ili wazazi wanunue wenyewe.
Pia
wanatakiwa kusimamia na kuhakikisha fedha inayotolewa na Serikali
inatumika kama ilivyokusudiwa kulingana na taratibu za fedha za Serikali
na kutoa takwimu na taarifa sahihi za idadi ya wanafunzi na mahitaji
mengine ya shule.
Kamati au Bodi za Shule
Wizara katika
waraka huo inataka kamati za shule kufuatilia na kusimamia matumizi ya
fedha zinazotolewa na Serikali ili ziweze kuleta tija; kuhakikisha kuwa
sera, nyaraka, maelekezo na miongozo ya Serikali inazingatiwa na kutoa
ushauri stahiki.
Kuwashirikisha wazazi, walezi, walimu na
wanafunzi katika maamuzi na maazimio ya masuala mbalimbali yanayohusu
maslahi na maendeleo ya shule kwa ujumla.
Pia waraka huo
umeainisha majukumu ya walimu ambao kazi yao kubwa ni kusimamia sera na
miongozo ya utoaji wa elimu bure. Wanafunzi ambao ndio walengwa wakuu wa
utoaji wa elimu pia wametakiwa kuhakikisha wanakuwepo shule katika
kipindi chote cha masomo.
-
Blogger Comment
-
Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments :
Post a Comment