SHERIA YA USIMAMIZI WA MIRATHI SURA YA 352 YA SHERIA ZA TANZANIA
1. SHERIA HII INASHUGHULIKA NA MAMBO YAPI NA INA LENGO GANI HASA?
Lengo kuu la sheria hii ni kutoa utaratibu wa kusimamia mali za marehemu
baada ya kifo chake ikiwamo kuhamisha umiliki wa mali hizo kutoka kwa
marehemu kwenda kwa watu wenye haki ya kuzipata mali hizo.Nia hasa ni
kwamba mali alizoacha marehemu zisibaki zikiharibika na kupotea bure,au
warithi halali au watu wenye maslahi na mali za marehemu,kwa mfano wale
wanaomdai hawapotezi haki hiyo, bali awepo mtu ambaye atazisimamia na
kuzigawa kwa wahusika wakiwamo wadai na kuepusha mgongano katika jamii
husika.Hivyo sheria inamuweka msimamizi wa kugawa mirathi husika na
mamlaka yake.
2. MAHAKAMA ZIPI ZINA MAMLAKA YA KUSIKILIZA MASUALA HAYA
Mirathi inaweza kufunguliwa katika mahakama mbalimbali kutegemea na sheria itakayosimamia mirathi husika.
v Kama sheria ya kimila itatumika katika kugawa mirathi basi shauri la
kuomba usimamizi wa mirathi litafunguliwa katika Mahakama ya
Mwanzo.Msimamizi wa mirathi anatakiwa airidhishe mahakama kwamba
marehemu kutokana na maneno yake,mfumo wake wa maisha au maandishi
aliyoacha,alionyesha nia kwamba mirathi yake alitaka iendeshwe kwa
kufuata sheria za kimila.
v Kama sheria itakayotumika ni ya kiisilamu basi shauri la kuomba
usimamizi wa mirathi litafunguliwa Mahakama ya Mwanzo.Msimamizi wa
mirathi anatakiwa airidhishe mahakama kwamba marehemu kutokana na maneno
yake,mfumo wake wa maisha au maandishi aliyoacha,alionyesha nia kwamba
mirathi yake alitaka iendeshwe kwa kufuata sheria za kiislamu.
v Kama sheria itakayotumika kugawa mirathi ni ya Serikali basi mahakama
wilaya,mahakama ya hakimu mkazi na mahakama kuu zinahusika kutegemea
thamani ya mali alizoacha marehemu.
· Thamani ya mali yote aliyoiacha marehemu isiyoondosheka isiyozidi
shilingi milioni 5 (Mfano nyumba, mashamba) na inayoondosheka isiyozidi
shilingi milioni 3 (mfano magari) mirathi ya aina hii inafunguliwa
Mahakama ya Mwanzo.
· Thamani ya mali yote aliyoiacha marehemu isiyohamishika isiyozidi
shilingi milioni 12 na inayohamishika isiyozidi shilingi milioni 100
mirathi hii inafunguliwa katika Mahakama ya Wilaya ama ya Hakimu Mkazi.
· Thamani ya mali inayozidi shs millioni 150 mirathi hii inafunguliwa mahakama Kuu.
3. SHERIA NA SIFA ZA KUWA WASIMAMIZI WA MIRATHI.
A] Ndugu wa marehemu na wale wenye maslahi na mirathi ya marehemu,kwa
mfano wale ambao wanatarajia kupata sehemu ya mirathi ya marehemu.
B] Mtu au watu wanaomdai marehemu,Mtu huyu hufungua mirathi pale ambapo
ndugu wa marehemu wameshindwa au hawataki kufungua mirathi.
C] Kkabidhi wasii mkuu, huyu au hii ni ofisi ya serikali ambayo
hujihusisha,Pamoja na mambo mengine,usimamizi wa mirathi,endapo itaombwa
na mtu yeyote.
D] Muwakilishi wa kisheria mtu aliyetajwa kama msimamizi wa mirathi [mtu aliyepewa power of attorney]
E]Mtu yeyote ambaye mahakama kwa kuangalia vigezo mbalimbali vikiwamo
udugu,maslahi ya muhusika katika mirathi hiyo,usalama wa mali za mirathi
pamoja na uwezekano wa kuisimamia vizuri,anaweza kuteuliwa na mahakama
VILEVILE Sheria imetoa baadhi ya vigezo ambavyo mtu lazima awe navyo ali apate usimamizi wa mirathi
I]awe mtu mzima
Ii]awe na akili timamu
4. KUNA NAMNA NGAPI ZA UTOAJI WA MAMLAKA YA USIMAMIZI WA MIRATHI
Namna ya kutoa usimamizi wa mirathi hutegemea jinsi marehemu
alivyojiandaa kukutana na kifo chake,kuna wengine huacha wosia na
wengine huwa hawaachi wosia.
A] KAMA KUNA WOSIA
Kama kuna wosia usimamizi wa mirathi hupewa mtu yule tu aliyetajwa
kwenye wosia,mtu huyo anaweza kuwa ametajwa moja kwa moja au kwa hali
halisi ilivyojionyesha kwenye wosia kwamba lazima atakuwa ni yeye.Hivyo
kuandika wosia ni nafasi pekee ya kuchagua msimamizi wa mirathi.
Vile vile mtoa wosia anaweza kuchagua mtu zaidi ya mmoja kusimamia
mirathi yake.Ikumbukwe kuwa kuna wosia za aina mbili.Ya kwanza ni wosia
wa maandishi na wa pili ni ule wa maneno.Wosia wa maneno ni lazima
uthibitishwe kwa ushahidi wa wahusika ambao ulitolewa mbele yao.Pale
ambapo mahakama itajiridhisha na uwepo wa wosia na ikatoa amri ya
usimamizi itakuwa imethibitisha usahihi wosia husika.Wosia wa maandishi
nao lazima uthibitishwe angalau kwa kuleta mtu aliyeshuhudia ukiandikwa
ili athibitishe kwamba marehemu alikuwa na akili timamu wakati akiandika
wosia huo na hakulazimishwa na mtu yeyote.
B] WOSIA ULIOMBATANISHWA NA BARUA YA USIMAMIZI WA MIRATHI
Hii hutokea katika mazingira yafuatayo
i] Pale ambapo marehemu ameacha wosia lakini wosia huo haujamtaja mtu ambaye amarehemu alitaka awe msimamizi wa mirathi yake
ii] Pale ambapo watu wote waliotajwa na marehemu katika wosia kwamba
wasimamie mirathi yake wamekataa hoja hiyo au ni watu ambao kisheria
hawana uwezo wa kusimamia mirathi,kwa mfano mtoto,mtu asiye na akili
timamu
iii] Pale ambapo wasimamizi wote wa mirathi walitajwa katika wosia
wamefariki kabla mwandika wosia hajafariki au amefariki kabla ya
kumaliza kazi yake ya usimamizi wa mirathi.
Katika hali kama hii,lazima ndugu wakae wachague mtu ambaye
wamempendekeza kuwa msimamizi wa mirathi na watatakiwa waende mahakamani
na wosia huo ili wakaombe mahakama imthibitishe rasmi.Hapa ndipo amri
ya usimamizi wa mirathi ukiwa na wosia ulioambatanishwa na barua ya
usimamizi wa mirathi hutolewa.
C] KAMA HAKUNA WOSIA
Kama marehemu hakuacha wosia wowote,barua za usimamizi wa mirathi
zinaweza kutolewa kwa mtu yoyote ambaye kwa mujibu wa taratibu za
usimamizi wa mirathi zinazohusika katika mirathi hiyo[za kimila au za
kiserikali au za kiislamu] atakuwa ana haki ya kupata mali zote za
marehemu au sehemu ya mali hizo.Pale inapotokea mtu zaidi ya mmoja
ameomba usimamizi wa mirathi ya marehemu,mahakama itakuwa na utashi wa
kuchagua mmoja au mtu zaidi ya mmoja kusimamia mali za marehemu,na
katika kufanya hivyo mahakama inatakiwa kisheria iangalie mtu mwenye
maslahi makubwa zaidi naya karibu na mirathi hiyo kuliko yule mwenye
maslahi madogo.Vile vile kama itatokea kwamba marehemu alikuwa
anadaiwa,na hakuna ndugu aliyefungua mirathi ya marehemu mahakamani,basi
mdai ana uwezo wa kuomba kufungua mirathi husika
Mahakama inapoona kwamba ni muhimu au ni busara kumchagua mtu ambaye
katika hali ya kawaida asingechaguliwa kusimamia mirathi,mahakama,kwa
kuangalia ukaribu wa kiundugu,maslahi aliyonayo muhusika katika
mirathi,usalama wa mirathi husika na uwezekano wa mirathi hiyo
kusimamiwa vyema,itamchagua mtu huyo asimamie mirathi.
D] USIMAMIZI WA MIRATHI KWA MAMBO MAALUMU.
I] USIMAMIZI WA MIRATHI WAKATI SHAURI LIKIENDELEA KUSIKILIZWA
Inawezekana kwamba
-bado kuna ubishi mahakamani kuhusu uhalali wa wosia,au
shauri la kuomba kupata barua ya usimamizi wa mirathi kwa mtu ambaye hakuacha wosia bado linaendelea au
-shauri la kuomba mahakama izifute barua za usimamizi wa mirathi alizopewa mtu Fulani linaendelea ,
-mahakama ina uwezo wa kuteua msimamizi wa muda wa mali za marehemu huku
kesi ikiendelea mahakamani.Msimamizi huyu atakuwa na mamlaka kamili
kama aliyo nayo msimamizi ma kudumu wa mali za marehemu isipokuwa tu
haruhusiwi kugawanya mali za marehemu.Vilevile msimamizi huyu atakuwa
chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa mahakama. Ili muhusika apate
ruksa hii ni lazima atoe sababu za kuonesha dharura ya ombi husika na
umuhimu wakeSuala hili limekuwa likiwatatiza hasa hasa akina mama na
watoto.Inaweza kutokea watoto bado wanasoma shule na baba yao
akafariki.Baba ana mali nyingi pengine ana akaunti benki.Lakini pengine
ndugu au watu wowote bado wanabishana mahakamani kwamba ni nani ana haki
ya kusimamia mirathi.Ni mara nyingi inatokea mahakama inaruhusu akina
mama hawa kuchukua kiasi Fulani cha pesa kulipa ada za watoto
wao,kuwatibu,hata matumizi ya muhimu ya nyumbani bora tu wasijihusishe
na kugawa mali za marehemu.
ii] MTEULIWA WA KUSIMAMIA MIRATHI BADO ANA UMRI MDOGO
Pale ambapo mtu anayatakiwa kusimamia mirathi bado ana umri
mdogo,usimamizi wa muda hupewa mtu mzima ambaye atakuwa ameteuliwa na
mahakama kama mwangalizi wa mtoto na mali zake au kwa mtu yeyote ambaye
mahakama itaona anafaa mpaka pale muhusika atakapokuwa mtu mzima na kuwa
na uwezo wa kusimamia mali zake vizuri.
Iii] MTEULIWA WA KUSIMAMIA MIRATHI HANA AKILI TIMAMU
Pale ambapo mtu anayetarajiwa kusimamia mirathi hana akili
timamu,mahakama itamteua mtu ambaye atasimamia mirathi hiyo kwa muda na
kwa faida ya muhusika mpaka pale atakapokuwa na uwezowa kiakili wa
kuisimamia mirathi husika
Iii] USIMAMIZI WA MIRATHI KWA AJILI YA KUKUSANYA NA KUTUNZA MALI ZA MAREHEMU
Kama inaonekana ni muhimu kwamba mali za marehemu zikusanywe na
kuhifadhiwa pahal pamoja,mahakama inaweza kutoa usimamizi huo kwa mtu
yoyote ambaye anafaa ili afanye kazi hiyo ikiwa ni pamoja na kulipa
madeni lakini haruhusiwi kugawa mali kwa warithi
-
Blogger Comment
-
Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments :
Post a Comment