TUNDU LISSU: Mpambanaji aliyeuanza uanaharakati utotoni
Apr 19, 2012
by Raia Mwema in Habari
JUNI 3, mwaka huu, Mwandishi Wetu, Godfrey Dilunga, alifanya mahojiano
kuhusu masuala mbalimbali na Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA)
ambaye pia ni mwanaharakati wa haki za binadamu, Tundu Lissu, jijini Dar
es Salaam. Yafuatayo ndiyo yaliyojiri kwenye mahojiano hayo.
Raia Mwema: Tuanze na historia yako kwa muhtasari.
Lissu: Niliishi maisha ya furaha sana ya utoto. Tangu nikiwa shule ya
msingi ni kama vile nilikuwa mwanaharakati. Unajua shuleni kuna shughuli
nyingi sana kama kuchota maji kwa ajili ya walimu, kulima mashamba ya
walimu na kupanda. Nilikuwa nikiona haya mambo hayako sawa, lakini pia
kuna suala la kuwahi shuleni.
Sikumbuki kwa miaka saba ya shule
ya msingi, kama kuna siku nimewahi zile namba. Siku zote nilikuwa
mchelewaji na nimechapwa kweli.
Raia Mwema: Ni ukaidi wa makusudi?
Lissu: Siwezi kusema ni makusudi, lakini tatizo ni kuamka alfajiri saa
11 ili saa 12 niwe shuleni. Kwa hilo nilikuwa rebel (muasi). Pia
sikumbuki mahali ambako sikuwahi kubishana na walimu iwe primary school,
secondary school, iwe chuo kikuu, siku zote imekuwa hivyo.
Lakini vile vile nilizaliwa katika familia ambayo mijadala ya kisiasa
ilikuwa sehemu yetu. Baba yangu alisoma hadi darasa la sita, mama yangu
hakusoma kabisa.
Kila jioni tunasikiliza kwanza taarifa ya habari
na idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani; baada ya hapo ni mjadala mpaka saa
tano au sita, mjadala wa kisiasa kuhusu mwenendo wa mambo duniani.
Nilikuwa mtoto mdogo sana, lakini nilikuwa na ufahamu.
Nafikiri nilikuwa miaka sita au saba hivi.
Wakati nikiwa darasa la kwanza (1976), nilikuwa nafahamu karibu viongozi wote duniani na miji mikuu mashuhuri.
Raia Mwema: Kutokana na ufahamu huo, ni viongozi gani hapa nchini walikuvutia wakati huo?
Lissu: Ni swali gumu kidogo. Si rahisi sana kusema nilivutiwa na
Mwalimu Nyerere. Ukweli ni kwamba hapana, alikuwa sehemu ya mazungumzo
ya kisiasa nchini. Siwezi nikasema nilivutiwa sana na Mwalimu.
Raia Mwema: Unaposikia jina la Julius Nyerere kwa sasa, unakumbuka nini?
Lissu: Ni hotuba za Mwalimu Nyerere kuhusu vita dhidi ya Uganda. Wakati
huo nikiwa darasa la tatu mwaka 1978, nchi iko vitani tulichangishwa
(familia) ng’ombe.
Baba yangu alitoa ng’ombe watatu kama sikosei
ili kusaidia vita mpakani. Shuleni tuliimbishwa sana nyimbo kwamba Iddi
Amini ni nyoka; ingawa baadaye nimekuja kugundua kwamba inawezekana kuna
vitu vingine vingi hatukuambiwa kuhusu mgogoro wetu na Uganda.
Nakumbuka pia wakati huo tukiwa wadogo tulichimbishwa mahandaki.
Nilikuwa na miaka 10, nilishangaa tunachimba (mahandaki) nje ya nyumba
yetu halafu siyo marefu sana.
Lakini kuna kitu kingine
kilichotafsiri mtazamo wangu kuhusu serikali ambao sio chanya sana.
Nilipokuwa miaka kama sita hivi, nyumba yetu na wanavijiji wengine
zilibomolewa halafu tukaachwa tu. Kina mama wanalia, kila mtu analia;
halafu hawa watu wakavunja nyumba wakaondoka.
Raia Mwema: Hao wavunjaji walitumwa na nani?
Lissu: Unajua ukiwa na miaka 10 huulizi sana. Ni tukio ambalo haliwezi
kuondoka katika kumbukumbu zangu kwamba; serikali inaweza kufanya vitu
visivyo na akili (mantiki).
Sisi na wanakijiji wengine tumejenga
nyumba, ingawa pengine hazikuwa nzuri sana wao (serikali) wametubomolea
kwa jina la Operesheni Vijiji.
Baba yangu alikuwa Mwenyekiti wa
Kijiji wakati huo, baadaye (watendaji wa serikali) wakaja na kamba za
katani na wataalamu ili kupima namna ya kujenga nyumba za kisasa,
wanaita maendeleo.
Kwa hiyo, wazee wanatembea na kamba ya katani
wanapima namna ya kujenga nyumba za kisasa , zijengwe kwa mstari
ulionyooka. Lakini hatimaye hawakutujengea wala kutusaidia chochote.
Hali hiyo ilinifanya niamini kwamba pengine serikali haina watu wenye akili sana kama nilivyokuwa nikifirikia mwanzoni.
Raia Mwema: Ukiwa katika umri wa utoto, unakumbuka nini enzi za nchi kufunga mikanda na baa la njaa lililowahi kutokea?
Lissu: Kuna njaa ya mwaka 1974 serikali ilileta chakula kudhibiti njaa
hiyo, nakumbuka kuna kitu (chakula) kinaitwa burga ilikuwa sijaanza
shule baadaye tukaletewa ugali wa muhogo. Sisi kwetu tunakula muhogo wa
kuchemsha. Ilikuwa hali tofauti.
Raia Mwema: Tueleze safari yako kielimu, ilikuwaje…ngumu au nyepesi tu.
Lissu: Wakati wa Operesheni Vijiji ilitokea mvutano wa kuhama. Baba
yangu pamoja na wazee wengine walisafiri kutoka kijijini Singida wakaja
Dar es Salaam kulalamika.
Walilalamika kwamba tunatakiwa tuhame
kwenye kijiji chenye mashamba makubwa. Wakaja kupiga kelele na serikali
wakati huo iliwasilikiza.
Lakini ikaibuliwa hoja kwamba; tuhame
(kijiji) kwa sababu hakuna shule. Wakati ule, hoja ya vijiji vya ujamaa
ililazimisha kuwapo huduma za kijamii.
Sasa ili kukabili hoja
hiyo na tusiweze kuhamishwa, kuna mzee mmoja alijenga nyumba yake mpya,
akasema sitahamia ili iwe shule ya watoto. Kwa hiyo, tukaanza shule
lakini shida walimu.
Mmoja wa wadogo zake baba yangu wakati huo
alikuwa amemaliza darasa la saba, hana pa kwenda, wakasema atakuwa
mwalimu. Kuna mama mwingine mjanja mjanja kijijini, naye wakamwambia
atakuwa mwalimu.
Kwa hiyo, tukaanza darasa la kwanza Aprili 5,
1976. Shule za miaka ile zilikuwa zinaanza Januari, lakini ya kwetu
tulianza Aprili, kwenye nyumba ya tembe sio ya bati, na walimu wasio na
mafunzo yoyote.
Hatukuwa na vitabu, swali likawa tutaandikia
nini? Wazee wakachanga hela wakamtuma mtu Dar es Salaam aende kumtafuta
mtu anaitwa Abdallah Nungu, amueleze tatizo la vitabu shuleni.
Kwa hiyo, tukamsuburi kwa wiki mbili huyu bwana alete vitabu. Akarudi na
boski kubwa la vitabu na vile vibao vya kuandikia, ingawa awali
tulikuwa tukiandika chini (ardhini). Hivyo ndivyo tulivyoanza shule
wengine.
Lakini hilo lilikuwa darasa la kwanza kwenye hiyo nyumba
ya mzee. Tatizo likajitokeza ni darasa la pili litakaa wapi, kwa sababu
ilibidi darasa la kwanza wengine waanze.
Nyumbani kwetu baba
alijenga nyumba jirani na mdogo wake, lakini huyo mdogo wake hakuwa
akiishi hapo kijijini alikuwa Moshi, nyumba yake haikuwa ikikaliwa.
Mzee akasema darasa la pili hilo hapo (nyumba ya mdogo wake). Kwa hiyo,
darasa la pili tukahamia kwetu (nyumbani). Natoka mlango huu, naingia
mlango wa pili niko darasani. Baada ya hapo, tukaanza ujenzi wa shule
ambayo ikaitwa Shule ya Msingi Mahambe.
Raia Mwema: Serikali haikutoa mchango wowote katika hatua za awali za ujenzi?
Lissu: Hatukusaidiwa na serikali katika ujenzi. Ilikuwa asubuhi
tunakwenda shule, saa nane tunaporudi (shule) tunabeba vibuyu na ndoo za
maji pamoja na mama zetu kupeleka eneo la kufyatulia matofali; shughuli
iliyokuwa ikifanywa na baba zetu.
Mwaka mzima tumefyatua
matofali na baadaye kuanza ujenzi. Kule kwetu kuna Wakatoliki wengi,
pale eneo la ujenzi (wa shule) kulikuwa na padre anapita kwenda
kusalisha kijiji cha jirani kila Jumatano. Kila akipita anakuta ujenzi
unaendelea na watoto wanasaidia.
Huyo padre anaitwa Charles ni
mu-Irish, kila siku anapita pale anakuta watoto na wazazi wanafanya
kazi, nadhani alikuwa akijiuliza kuna nini?
Siku hiyo akasimama.
Alikuwa anatumia pikipiki kubwa….sijui ni kubwa (pikipiki) kweli au mimi
ndiye nilikuwa mtoto na kuiona kubwa.
Akauliza, akaambiwa
tunajenga shule. Akauliza serikali iko wapi? Akaahidi tukishamaliza
ujenzi, ataleta mafundi kukamilisha kwa kuweka bati, ikaitwa Shule ya
Wazazi.
Darasa la tatu tukaingia sasa kwenye darasa zuri na bora.
Kuanzia hapo, kila mwaka nilipokaa pale shule ya msingi tulikuwa
tunajenga darasa moja moja, hadi tulipomaliza mwaka 1979 tunaingia
darasa la tano ndiyo kwa mara ya kwanza ikaitwa Shule ya Msingi Mahambe,
na tutakaletewa mwalimu wa serikali.
Kwa hiyo, kati ya vyuo
vikuu vyangu, chuo kikuu cha kwanza ni hicho….miaka minne ya kufundishwa
na walimu wasio na mafunzo yoyote.
Siku hizi nikipita
nikiwaambia watu shule niliyosomea na walimu walionifundisha, hawaamini.
Tulifundishwa na wanakijiji kabisa wasio na mafunzo! Serikali
ilipoanzisha mpango wa UPE wale walimu walijiendeleza, wakaenda vyuoni
na wapo ambao wamekuwa waalimu wanataaluma.
Raia Mwema: Hayo ni ya shule ya msingi, tueleze ya sekondari, unakumbuka nini hasa?
Lissu: Cha kwanza nimetoka nje ya kwetu (Singida), nimeenda kusomea
Ilboru Sekondari, Arusha. Pale (Ilboru) maisha yalikuwa mazuri na
nilikuwa mdogo kuliko wengine wote (wanafunzi).
Sikuwahi kuwa
kiongozi shuleni, na sikutaka uongozi. Viongozi wakati ule tuliwaita
manyoka kwa sababu wanapeleka habari kwa walimu.
Lakini baadaye
nilipoingia kidato cha tano na sita, Galanos Sekondari (Tanga), nilipewa
uenyekiti wa Kamati ya Taaluma, lakini baada ya miezi sita hivi
nikagombana vibaya sana na mwalimu wa taaluma, ikabidi nivuliwe
madaraka.
Raia Mwema: Mlitofautiana katika jambo gani na mwalimu wa taaluma?
Lissu: Ni msimamo tu. Ilitokea kwamba mwaka 1988 niko kidato cha sita,
sasa kidato cha nne na cha sita kila mwaka hufanya graduation
(mahafali). Wakati huo, hasa Galanos na shule nyingi za sekondari, disko
hazikuwa nyingi (mara kwa mara) kama sasa.
Kipindi cha kwenda
kucheza disko ilikuwa wakati wa graduation. Sasa walimu wakaamua watoto
wa kidato cha nne hawatakwenda kucheza disko. Mimi niko kidato cha sita,
sasa tulipanga kwenda disko Korogwe Girls. Wakaamua (walimu) kidato cha
nne hawatakwenda Korogwe Girls, badala yake waletewe taarabu.
Sikukubaliana, nikaandika makala inahoji uamuzi huo. Title yake
naikumbuka hadi leo, inasema; “taarab for who’s benefit?” – taarabu kwa
faida ya nani?
Halafu tukafanya mpango (wanafunzi) ikabandikwa
kwenye mbao za matangazo shuleni, sikuandika jina langu halisi. Walimu
wakauliza, wakapeleleza nani anaweza kuandika vitu kama
hivi?….wakanikamata.
Nikatuhumiwa kuleta uchochezi,
nikasimamishwa shule, baadaye walinirudisha. Lakini kwa ujumla miaka ya
sekondari ilikuwa mizuri, hapakuwa na njaa kama wakati huu.
Raia Mwema: Baada ya kuhitimu kidato cha sita, nini kilichofuatia?
Lissu: Nikaenda JKT Mbeya, kwanza nilipelekwa Mafinga, lakini sikukaa
tukapelekwa Mbeya operesheni yangu inaitwa; Operesheni ya Programu ya
Chama, mwaka 1989.
Raia Mwema: Unakumbuka nini kuhusu enzi za JKT?
Lissu: Ninachokumbuka mjadala wa vyama vingi ulikuwa umeiva na CCM
hawataki vyama vingi. Ilikuwa mwaka 1989/1990, kwa Katiba ya CCM wakati
huo, kulikuwa kuna mkoa unaitwa Mkoa wa Majeshi, ulikuwa mkoa sawa na
mingine katika chama.
Kwa hiyo, wakatuma wajumbe wao wa Mkoa wa Majeshi kutembelea kambi zote za jeshi na JKT Tanzania nzima, kueleza msimamo wa CCM.
Waliokuja Itende JKT kwetu nawakumbuka ni Omari Mahita wakati huo ni
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Kanali Andrew Shija na mtu mwingine
simkumbuki.
Nawakumbuka Kanali Shija na Omari Mahita kwa sababu
walijenga hoja kwamba haya mageuzi (vyama vingi) hayatuhusu kwa hiyo
tusishabikie yasiyotuhusu; eti yanayowahusu Wazungu, Ulaya Mashariki na
kwingine.
Nakumbuka nilipambana vibaya sana na Omari Mahita
kwenye huo mkutano. Nilisimama kuuliza maswali nikitambua kuwa kabla
hawajaja, Mwalimu Nyerere alihutubia mkutano wa Baraza Kuu la Vijana wa
CCM, Mwanza na akasema wanaodhani mageuzi ya Ulaya Mashariki hayatuhusu,
ni wajinga.
Kwa hiyo, nikamuuliza RPC Omari Mahita nikamwambia
kwamba Mwalimu Nyerere alisema wanaofikiri mageuzi ya Ulaya Mashariki
hayatuhusu ni wajinga, na wewe umekuja na timu yako unatuambia haya
mambo ni ya Wazungu hayatuhusu.
Sasa mjinga ni Mwalimu Nyerere aliyesema yanatuhusu au nyie ambao mnatuambia kwamba hayatuhusu?
Raia Mwema: Bila shaka ulitumbukia katika uhasama wa ghafla na meza kuu. Hali ilikuwaje?
Lissu: Omari Mahita ni mweupe sana, basi, ghafla akabadilika rangi
akawa mwekundu. Ikawa makamanda kadhaa wakasimama tayari kumshughulikia
huyu serviceman…maana nilishapita ukuruta. Wakasimama kutaka
kumshughulikia anayetukana maofisa wa jeshi.
Lakini kanali Shija
(marehemu sasa) akasimama akanitetea. Akasema; hoja ya serviceman ni
sahihi kabisa, Mwalimu ndivyo alivyosema. Kwa hiyo, hatuwezi….kusema
hayatuhusu. Maana yake tayari nilianza kusakamwa pale… akasema ni kweli
hatuwezi kukwepa haya mawimbi na upepo. Shija akapiga siasa, na hatimaye
akaniepushia kibano.
Raia Mwema: Kwa hiyo makamanda wenyewe kwa wenyewe walitofautiana mbele yenu?
Lissu: Walitofautiana na baada ya hapo, hakuna ofisa wa JKT aliyenigusa
tena. Wengi baada ya hapo wakaamini mimi ni usalama wa taifa.
Maisha yakawa mazuri. Hakuna aliyenigusa kwa sababu kama nimezungumza
vile na kanali wa jeshi, kwa sababu mkuu wa kambi mwenyewe hakuwa
kanali, alikuwa luteni kanali, sasa mimi nimetetewa na Kanali Shija. Kwa
hiyo nilikuwa nakula shushi (mambo mteremko).
Baada ya hapo
nikaenda Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Miaka ile ulikuwa huendi
chuo kikuu kama si mwanachama wa CCM na sehemu ya mafunzo unayopata JKT
ni pamoja na itikadi ya CCM na mnapomaliza mafunzo mnakabidhiwa pia kadi
za chama. Kwa hiyo, nilikuwa mwanachama wa CCM na hiyo ni muhimu watu
wakafahamu.
Lakini nilikuwa mwanachama kwa sababu tu nilitaka
kusoma. Ndivyo maisha yalivyokuwa na baada ya hapo. Nilipoingia chuoni
kadi haikuwa na kazi sana kwangu. Siku ya kwanza chuo kikuu hadi
naondoka, mijadala yote nilikuwa mstari wa mbele kabisa pamoja na kwamba
sikuwahi kuwa kiongozi.
Raia Mwema: Katika mijadala yenu chuoni hasa ile mikubwa, hoja gani unakumbuka zilitikisa uongozi au hata nchi?
Lissu: Wakati huo, dunia na nchi ilikuwa ikibadilika, hatukuwa tayari
tena kutawaliwa na mfumo wa chama kimoja, eti usipokuwa na kadi ya chama
huendi chuo. Nikiwa mwanafunzi, uchangiaji wa gharama za shule ulianza
wakati huo.
Nilikaa mwaka mzima nyumbani kabla ya kuingia chuo kikuu kwa sababu mwaka 1989 wanafunzi wa UDSM waligoma, chuo kikafungwa.
Pamoja na kwamba sikuwa sehemu ya huo mgomo wakati huo nilikuwa JKT,
lakini madhara ya mgomo yalinigusa kwa kukaa nyumbani mwaka mzima.
Nilipojiunga chuo mwaka 1991, tayari vuguvugu lilikuwa kubwa sana. Na
upinzani dhidi ya uchangiaji gharama za elimu ulikuwa mkubwa sana.
Raia Mwema: Mliguswa vipi na tukio la kumdhalilisha Rais Mwinyi wakati ule chuoni UDSM?
Lissu: Chuo kilifungwa kutokana na tatizo hilo mwaka 1989. Ni tukio
lililotugharimu ambao ndiyo tulitaraji kwenda kuanza masomo. Tulikaa
nyumbani mwaka mzima.
Raia Mwema: Katika changamoto za mageuzi chuoni, baadaye ulijiunga na chama gani baada ya mfumo wa vyama vingi kuruhusiwa?
Lissu: Kama nilivyosema, nimezaliwa rebel , na hivyo haikuwa ajabu hata
kidogo mimi kujiunga na chama cha upinzani ambacho kilivutia wasomi –
NCCR-Mageuzi. Ilikuwa ni hatua inayotegemewa.
Nisingeweza kuwa
CCM au CHADEMA kwa sababu kilikuwa chama kisichokuwa na msimamo
mkali….hawa watu ni waoga, wanaogopa kuweka msimamo mkali. Ni kama chama
cha kibepari hivi na mimi kimsimamo nimekuwa Mjamaa wa mrengo wa
kushoto kabisa.
Raia Mwema: Uchaguzi wa kwanza baada kuruhusiwa vyama vingi mwaka 1992 ulifanyika 1995. Ulishiriki vipi uchaguzi huo?
Lissu: Ingawa jimboni kwetu (Singida Kusini wakati huo) mwanzo hapakuwa
na uchaguzi wa vyama vingi, lakini ilikuwa sehemu ya changamoto
kisiasa, hata wabunge waliokuwa wakichaguliwa walidumu kwa muhula mmoja
tu.
Sasa ghafla tukawa na demokrasia pana zaidi – vyama vingi,
lakini kwenye uchaguzi huo (1995) ikaelekea CCM itapita bila kupingwa.
Kwa hiyo nikajitokeza kugombea ubunge jimbo la Singida Kusini.
Lakini wakati naanza mchakato wa kuwa mgombea, nikapata scholarship ya
Serikali ya Uingereza kwenda kusoma Master’s (Uzamili). Nikaenda shule
kuripoti, nikawaambia narudi nyumbani kujaribu ubunge, nikishindwa
nitarudi.
Nikatoka Uingereza kuja kugombea ubunge mwaka 1995,
nikiwa na miaka 27. Nikarudi shule baada ya kushindwa. Safari yangu ya
kisiasa ilianza kujitokeza kipindi hicho.
Nikamaliza shule yangu
mwaka 1997, nikaoa na nikahamia Dar es Salaam (kutoka Arusha alikokuwa
akifanya kazi kama mwanasheria ofisi binafsi).
Raia Mwema: Katika harakati zako, tukio gani kubwa unakumbuka lilikutia msukosuko au kuibua katika jamii?
Lissu: Tukio la kwanza kubwa ilikuwa ni mradi wa ufugaji kamba delta ya
Rufiji. Mradi wa Mzungu mmoja wa Ireland anaitwa Reginald Nolan.
Alipewa na Serikali ya Mkapa hekta 20,000 ili atengeneze mabwawa ya
kufuga kamba kwenye delta ya Rufiji katika maeneo ambayo yana vijiji
karibu vinane, watu walima na kuishi, kuna msitu ya mikoko pale. Yote
ile Reginald Nolan akapewa ili atengeneze mabwawa. Sisi kama watetezi wa
mazingira kupitia Chama Cha Wanasheria wa Mazingira – LEAT, tulishikia
sana bango mradi wa Rufiji.
Tulifanya kazi kubwa. Niliratibu
kampeni ya kimataifa kwa kila njia, ikiwamo mitandao ya kimataifa ya
wanaharakati kuupinga mradi huo.
Hatimaye, Benki ya Vitega Uchumi
ya Ulaya (European Investment Bank) iliyokuwa itoe mkopo kwa Nolan
ambao ungedhaminiwa na Serikali ya Tanzania, wakasema hawatatoa mkopo na
kwa hiyo, mradi mzima ukasambaratika.
Niliwahi kushiriki mdahalo
kwenye kituo cha televisheni nchini kuhusu mradi huo wa kamba, nikiwa
mimi, mmiliki wa mradi na mwandishi wa habari wa siku nyingi, James
Mpinga. Kwa mara ya kwanza ndipo nilipoanza kuonekana kwenye televisheni
katika kipindi cha Hamza Kasongo Hour, Oktoba 1998.
Tuliwasambaratisha kila mahali. Tukapata nyaraka za Baraza la Mawaziri
zilizosema mradi ni wa hovyo, lakini umepitishwa kinyemela.
Raia Mwema: Katika mchakato mzima wa harakati hizo, uliwahi kukumbwa na vitisho vya aina fulani?
Lissu: Vitisho vingi. Unaweza kufika ofisini ukakuta bahasha yenye ujumbe wa vitisho imepenyezwa chini ya mlango.
Baada ya hapo Machi, mwaka 1999, kuna kampuni moja wenye ginnery (kinu
cha kuchambua pamba). Ni kampuni ya ki-Swisi. Wakaja ofisini kwetu
(LEAT) wakaomba tuwafanyie utafiti juu ya madhara wanayoweza kupata
kutokana na mgodi uliokuwa ukijengwa Geita. Walitaka kubaini kama
shughuli za mgodi zitaathiri shughuli zao za kusafisha pamba.
Kwa
hiyo, nikapewa hiyo kazi. Nikasafiri kwenda Geita, asubuhi yake (baada
ya safari) wenyeji wangu wakanipeleka wanakojenga mgodi. Nikakuta vijiji
vinabomolewa kwa magreda na mbele yake wametangulia askari wenye
bunduki. Kijiji kile kilipitiwa na barabara, sasa upande wa pili wa
barabara yuko Mkuu wa Wilaya, Halima Mamuya, OCD na maofisa wengi.
Mkuu wa Wilaya ya Geita ameshika kipaza sauti, anawaambia wanakijiji
kwamba niliwaambia mlipwe fedha (fidia) mmekataa, sasa mtajua mtakwenda
wapi.
Pale kwenye shimo kubwa lenye kina cha Kilomita kama tano wanakochimba dhahabu ndipo kilipokuwapo kijiji cha Mtakuja.
Nilishuhudia mgodi wa kwanza ukianzishwa kwa kuharibu kijiji ambako
kulikuwa na makazi pamoja na mazao…mahindi yanayoelekea kukomaa, na
wakati huo nchi ilikuwa imekumbwa njaa kwa sababu mwaka uliopita
kulikuwa na mvua za el-nino.
Hali ile ilinikumbusha wakati wa
operesheni vijiji ambako nyumba yetu na za wanavijiji pamoja na mashamba
viliharibiwa. Nilishangaa serikali kuharibu mashamba ya chakula.
Nikaandika ripoti yangu, nikawapelekea wenye kinu cha pamba na
kupendekeza kwamba tunahitaji ginnery kukaa na wananchi kijiji ili
kupambana na uhalifu huo.
Nikawaambia nyie mna hela, wanakijiji
watawapa ile human element, idadi ya watu ambao wanaathiriwa.
Ukizungumza athari, ukaonyesha watu wanabomolewa ina value kubwa sana
katika mapambano. Kwa hiyo, wanakijiji mkiwaacha wakasambaratishwa, hata
nyinyi hamtabaki.
Wakaniambia sisi ni wawekezaji, nikawaambia
wenzangu katika LEAT kwamba ugomvi mkubwa katika miaka inayokuja ni
ugomvi wa madini.
Kwa hiyo, kutoka Geita kwenda Bulyanhulu ni
mwendo wa dakika 45. Katika kuchunguza makampuni ya madini yanafanya
nini kwa wananchi, kitu cha kwanza utakachokutana nacho ni Bulyanhulu.
Ndio eneo ambalo kulitokea maafa makubwa zaidi.
Mwaka 1999
nikapata nafasi kwenda Marekani kuwa mtafiti katika taasisi ya World
Resource Institute kwa miaka mitatu. Nikawaambia World Resorce Institute
nitafanya kwa sharti moja; kwamba kazi niliyoanza kuifanya katika LEAT
ya madini niendelee nayo.
Nikaondoka kwenda Marekani Septemba
1999 na kwa miaka mitatu yote mnayojajua juu ya Bulyanhulu yalipatikana
katika kipindi hicho. Karibu kila mwezi nilirudi Tanzania kuendelea
kutafiti suala hilo la Bulyanhulu.
Tulipata ushahidi wa picha za
video na nyingine unaothibitisha kwamba watu wengi waliuawa. Hizo picha
ni za jeshi la polisi na kampuni yenyewe.
Tulikuwa kila
tunapopata video hizo tunazitangaza hadharani. Mwaka 2001 tulifanya
press conference kubwa Maelezo kuthibitisha kwamba tunao ushahidi wa
picha za video zinazothibitisha mauaji hayo kutokea.
Nilikuwa
mimi na Rugemeleza Nshala. Baada ya mkutano huo, mimi nikaondoka kurudi
Marekani. Lakini huko nyuma, baada ya tarehe 23, Polisi wakavamia ofisi
zetu za LEAT na nyumbani kwangu wakitafuta huo ushahidi. Na wakati huo
Jeshi la Polisi likasema huyu mtu ametoroka, anatafutwa na Interpol, kwa
hiyo akamatwe. Wenzangu baadaye walikamatwa.
Niliporudi Marekani
walinikamata na kuniweka kituo kikuu cha polisi Dar es Salaam.
Nilipokuwa kituoni humo nilifanya ujanja nikaingia na simu na nikafanya
mahojiano na magazeti ya Canada na Marekani usiku kucha. Kesho yake
ilikuwa sikukuu ya Krismasi. Nikafuatwa na polisi, nikaambiwa napelekwa
mahakamani.
Raia Mwema: Tueleze kujiunga kwako na CHADEMA, kulikuwaje?
Lissu: Kujiunga na CHADEMA mwaka 2004 sababu ilikuwa Tarime na suala la
kampuni za madini. Harakati za madini Tarime nilizianza mwaka 2003.
Wakati ule mtu aliyenipokea Tarime ni marehemu Chacha Wangwe. Nilimkuta
ana kesi 10 za jinai wakati huo akiwa diwani wa CHADEMA. Akaniambia;
wanataka kunifunga hawa…nikamwambia hawawezi, wanakutisha tu.
Alisumbuliwa sana, na Tarime ilikuwa inatisha kama ilivyo leo. Mbowe
akanipigia simu akaniomba nisaidie kisheria kumtetea Wangwe, chama
kitagharimia usafiri. Kwa hiyo, nikaanza kazi ya kuwapa huduma ya
kisheria na katika kipindi cha miezi minne nimetoa gerezani watu 366
waliokuwa wanatumikia vifungo.
Siku moja Mbowe akaniambia
nitafute watu wengine wanataaluma ili wajiunge na CHADEMA. Nikamuuliza
kwa nini unafikiria mimi ni mwanachama wa CHADEMA? Alikuwa miaka yote
anafikiria mimi ni mwenzao, kumbe mimi ni NCCR-Mageuzi.
Akauliza
kwa nini si mwanachama wa CHADEMA? Nikamwambia hujawahi kunipa sababu za
kwa nini niwe mwanachama wa CHADEMA. Kama unataka niwe, niambie tu.
Kwa hiyo, hivyo ndivyo nilivyoingia CHADEMA. Kwa maisha yangu kwa
historia yangu na msimamo wangu, mimi ni mwanahakarati, na pengine Rais
Kikwete hakosei sana anaposema vyama vingine ni vya wanaharakati.
Raia Mwema: Unazungumziaje nafasi yenu Bungeni, hasa ikizingatiwa suala la idadi na ubora wenu?
Lissu: Bunge kama unaelewa sawawa linakupa nafasi ya kuibua mijadala.
Siku zote sasa nimeelewa kwamba Bunge si mahali pazuri pa kutatulia
migogoro, lakini ni mahali pazuri pa kuzungumzia na ku-mobilise nguvu ya
umma. Hayo matatizo ya kisiasa au kikatiba, hayatatuliwi bungeni
isipokuwa yanazungumzwa.
Suala la wingi, kwa maana ya idadi au ubora wa wabunge, bila kujali idadi lina umuhimu wake.
Kwa mfano; inapofika wakati wa kupitisha sheria au bajeti, hatuwezi
ingawa tunao wabunge bora zaidi na wajenga hoja wazuri. Kwa hiyo, hapo
‘ujinga wa wengi’ ndipo unaposhinda. Kama unaitumia nafasi hiyo bungeni
vizuri, kama ambavyo tumekuwa tunafanya, hiyo itakuwa inatusaidia
kujenga nguvu kubwa nje ya bunge. Inategemea unatumiaje hiyo fursa ya
Bunge.
Raia Mwema: Ulikuwa Tarime hivi karibuni. Wako wanaohoji ulikwenda kutafuta nini wakati ni eneo lenye mbunge wake.
Lissu: Labda niwajibu hao wajinga wasiojua nilikuwa nafanya nini
Tarime. Kwa historia yangu na Tarime, ilikuwa ni wazi ningeenda Tarime
baada ya kutokea masuala haya (mauaji) na ndugu zao kukataa kuwazika
hadi uchunguzi. Ningekuwa sio mbunge pia ningekwenda Tarime. Nina
historia ndefu ya mapambano ya kudai haki Tarime.
Yaliyotokea
yanafamika – tulikamatwa na kuwekwa kwenye selo Tarime, tumeshtakiwa. Ni
hali halisi ya Tarime. Ni eneo la vita, ni janga la kitaifa kama
nilivyoeleza baada ya kuachiwa kutoka gerezani.
Tarime ya leo ni
mbaya kuliko Tarime ya 2003 nilipokwenda kwa mara ya kwanza ambapo mamia
ya watu wa Nyamongo walikuwa gerezani. Tarime ya leo ni ya mauaji
yanayofanywa na jeshi la polisi. tangu tuwashinde (CCM) uchaguzi. Mauaji
ya kwanza Tarime yalifanyika Julai 20, 2005. Hadi kuua hawa wa juzi
watano, sasa wamefikia watu 28 waliouawa kwa kupigwa risasi mchana
kweupe.
Raia Mwema: Lakini kiini cha tatizo nini? Je, ni mwekezaji au jeshi la polisi?
Lissu: Tatizo ni mwekezaji, polisi na Serikali ya Tanzania. Kusingekuwapo mwekezaji, watu wasingeuawa.
Raia Mwema: Lakini kama tatizo ni pamoja na polisi au serikali kuna migodi mingine mauaji hayaendelei kama Tarime?
Lissu: Katika sekta ya madini unakuja na umwagaji damu. Bulyanhulu,
Tarime, Geita, Nzega hakuna mahali ambapo wawekezaji wameweka mgodi wa
dhahabu wa kisasa bila kuangamiza uchumi wa wenyeji, bila kuwaondoa kwa
mabavu ya kijeshi.
Raia Mwema: Kifanyike nini?
Lissu: Ni
mambo mawili ya kuchagua. Kwanza, je, tunataka huyo anayeitwa mwekezaji
achume mali na inunuliwe kwa damu za Watanzania? Inunuliwe kwa
Watanzania kukosa haki na kwa uchumi wa Watanzania kusambaratishwa? Au
tuamue kwamba maisha ya Watanzania ni bora zaidi kuliko dhahabu.
Kwa maoni yangu, haiwezi bei ya dhahabu ikawa sawa na maisha ya mtu
mmoja. Watanzania wameshauwa kwa risasi na kwa kunywa maji ya sumu
yanayotokana na mwekezaji. Tarime imejaa vijana wanaoshitakiwa kwa kesi
za ugomvi na mgodi, lakini sasa hivi wanashtakiwa kwa kesi za mauaji au
uhalifu wa kutumia silaha!
Wakati nakwenda Tarime kwa mara ya
kwanza, kesi zilizokuwa zikifunga watu zilikuwa uchochezi na kuvamia
eneo la mgodi, lakini leo kesi za Tarime ni mauaji. Hata ukikamatwa kwa
kurushwa jiwe ambalo halijampiga mtu yeyote, utashtakiwa kwa mauaji au
uhalifu wa kutumia silaha!
Na unashtakiwa kwa hayo makosa mawili kwa sababu huwezi kupewa dhamana. Kwa hiyo, polisi wasipofanya upelelezi utafia gerezani.
Nilikamatwa Tarime nikakaa gerezani. Naweza kuthibitisha kuwa Tarime kuna watu zaidi ya 400 wanaokabiliwa na kesi za mauaji.
Sasa njoo huku ambako hakuna mgodi, leo biashara ya teksi Tarime mjini
ni biashara ya mapolisi kwa sababu wafanyabiashara wa kawaida pale
mjiini aidha wako gerezani wakikabiliwa kwa mauji au wengine wameuawa.
Selo niliyofungwa mimi Tarime inatumika kwa kitu kimoja tu, nimeambiwa
kuna watu wengi sana wameuawa, wameumizwa sana. Kuna mtu mmoja amepigwa
risasi tano miguuni kwenye kituo cha polisi na mkononi amepigwa risasi
mbili, na mkono umekatwa.
Kuna watoto. Kuna mtoto wa miaka 12
selo niliyolala mimi. Bunge hili limepitisha sheria mwaka juzi, sheria
ya mtoto inayosema mtoto wa miaka 18 hawezi kupata adhabu ya kifungo.
Huyu mtoto ana miaka 12 anakaa kwenye gereza na wafungwa watu wazima
waliopatikana na hatia. Napeleka hoja binafsi bungeni kuomba iundwe
kamati teule ya Bunge kuchunguza suala hili.
-
Blogger Comment
-
Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments :
Post a Comment