Juma lililopita Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) liliaga timu
ya Taifa ya Vijana Chini ya umri wa miaka 15 (U15) ikianza ziara yake
ya Afrika Mashariki kuanzia kucheza na Burundi mjini Kigoma na baadaye
Kigali, Rwanda, Kampala, Uganda na mwisho Nairobi Kenya.
Bahati mbaya ziara hiyo itaishia Mwanza na Kigoma kufuatia Mamlaka ya
Kodi ya Mapato (TRA) mkoa wa Ilala kuzuia fedha kwenye akaunti zote za
Shirikisho kwa madai ya kulipwa kiasi cha Shilingi 1,637,334,000
(bilioni 1.6 tshs) ikiwa ni kodi kwa kipindi cha 2010 – 2013 sehemu
kubwa ikiwa ni makato kwenye mishahara (PAYE) ya walimu wa kigeni, Jan
Poulsen, Kim Poulsen na Jacob Michelsen na vilevile kodi ya ongezeko la
thamani (VAT) kwenye mchezo wa Timu ya Taifa (Taifa Stars) dhidi ya
Brazili uliofanyika mwaka 2010.
Walimu wa Timu za Taifa wamekuwa wakilipiwa mishahara na Serikali na
hivyo TFF haikuwajibika kuwakata kodi. Aidha, mchezo kati ya Tanzania na
Brazil ulisimamiwa na kamati maalum ya Serikali na fedha zake
hazikuingizwa katika akaunti za TFF.
Kutokana na hatua hii ya TRA shughuli nyingine za mpira zitakazohathirika nazo ni:
1. Kulipia madeni ya usafiri, chakula na posho za Timu za Taifa
zilizoshiriki mtoano wa kombe la Dunia na mashindano ya Afrika Mashariki
na Kati (Challenge Cup)
2. Program za mpira wa Wanawake na vijana zitalazimika kusimama.
3. Mashindano ya kombe la Shirikisho raundi ya pili iko kwenye hatihati kwani hakuna fedha za kugharimia michezo hiyo.
4. Mashindano ya Ligi Daraja la Pili (SDL) inayoendelea yatalazimika
kusimama vilevile. Mashindano haya TFF imekuwa ikiyaendesha bila
mdhamini.
5. Vifaa vya michezo (Mipira) kwa ajili ya shule za msingi na vituo vya
maendeleo (Regional Football Development Centres) vinatarajiwa kuwasili
nchini wakati wowote na TFF haitakuwa na uwezo wa kulipia usafirishaji
na ushuru wake.
6. Malipo ya gharama za kambi na karo kwa ajili ya vijana wa timu ya
Taifa ya vijana chini ya miaka 13 walioko shule ya Alliance Academy ya
jijini Mwanza.
7. Huduma za kiutawala ikiwa ni pamoja na utunzaji viwanja na majengo,
maji, umeme, ulinzi pamoja na mishahara na stahiki nyingine za
wafanyakazi
8. Mwelekeo na mwitikio mzuri wa wadhamini uko kwenye hatari ya kupotea
pindi mashindano na shughuli wanazozidhamini zitakapofubaa au kusimama
kabisa.
9. Mkutano Mkuu wa kawaida wa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) wa
Mwaka 2015 uliopangwa kufanyika Tanga 19-20 Desemba 2015 sasa una
hatihati ya kuweza kufanyika.
Hata hivyo, kwa kutambua umuhimu wa ulipaji kodi na wajibu wa Mamlaka ya
Mapato katika kuhakikisha kodi inakusanywa kwa ajili ya ustawi na
maendeleo ya Taifa,TFF ipo katika mawasiliano na TRA katika kutafuta
ufumbuzi wa kudumu wa suala hili ikiwa ni pamoja na kupitia upya
mahesabu ili kujua wajibu halisi (net liability) wa TFF na namna ya
kulipa au kulipwa kutegemea ulali wa mahesabu.
Hii si mara ya kwanza hili kujitokeza, lilijitokeza Oktoba 2012 na
shilingi 157,407,968 iliyokuwa mgawo wa vilabu kuchukuliwa na TRA.
Kufuatia tukio hilo, yalifanyika mazungumzo kati ya TFF na serikali
ambamo ilikubaliwa kwamba fedha hizo zitarudishwa TFF na mpaka sasa TFF
inafuatilia fedha hizo.
Kwa taarifa hii TFF inaomba utulivu kwa wanamichezo wote pamoja na
ushirikiano wa karibu kutoka katika vyombo vyote husika ikiwemo TRA na
wadau wengine ili jambo hili lipate ufumbuzi wa kudumu utakaoleta tija
kwa serikali ya awamu ya tano ikiwa ni pamoja na kuongeza uwekezaji
katika maendeleo ya mpira wa miguu na michezo kwa ujumla wake.

0 comments :
Post a Comment