CHAMA CHA CHADEMA NA UKAWA MH.
EDWARD NGOYAI LOWASSA.
ILANI NA KAMPENI YA UCHAGUZI MKUU
Jangwani-Dar-es-Salaam, 29 AGOST
Ndugu Wana Dar es salaam na
Watanzania wenzangu
1. Leo ni siku ya kihistoria. Baada ya
miaka ishirini na tano tangu mfumo
wa vyama vingi urejeshwe, vyama
vya upinzani wa CHADEMA, CUF,
NCCR na NLD umeungana chini ya
Umoja wa Katiba ya Wananchi
kupigania uchaguzi mkuu wa mwaka
huu na kuwa na mgombea mmoja
katika ngazi zote.
2. Miaka zaidi ya hamsini ya utawala
wa serikali za CCM na waasisi wake,
umekuwa utawala wa wachache
walio hodhi madaraka na mali za
nchi.
3. Leo tunaanza safari ya uhakika ya
kuleta mabadiliko ya kweli nchini.
1. Mabadiliko yaletayo neema na
kujenga upya mfumo wa
uchumi, haki na sheria nchini.
2. Mabadiliko ya kuimarisha
huduma za jamii kama elimu,
afya, maji na makazi.
3. Mabadiliko ya kuondoa
umaskini.
4. Mabadiliko tunayatoahidi ni
mabadiliko ya kurejesha
matumaini kwa Watanzania
kwa kubadili hali zao za
maisha.
4. Kila mwaka hali na ubora wa maisha
ya Watanzania imeshuka wakati
tunaambiwa kuwa pato laTaifa
linakuwa.
5. Lakini Watanzania wanachotaka siyo
takwimu bali kuona kipato chao
kinakua, shule, hospitali na barabara
bora zinajengwa.
6. Wanataka kupata maji safi na
salama ya kunywa. Wanataka
makazi bora.
7. CHADEMA na UKAWA, tuna dhamira
ya kuleta mabadiliko ya kweli ili
kuona azma ya Watanzania tangu
uhuru ya kuondoa umaskini,
maradhi,na ujinga inahitimishwa.
8. Ili tufanye hivyo tuahitaji tufanye
mabadiliko ya fikra, uongozi, sera
na utendaji.
9. Leo Tanzania inakabiliwa na
changamoto nyingi za ki-uchumi,
kisiasa na kijamii. Changamoto hizi
ni matokeo ya sera za utawala wa
Chama kimoja wa miaka hamsini.
Sote ni wahanga wa siasa na sera
hizi.
10. Miaka Hamsini ya CCM imetosha.
Tunataka mabadiliko na siyo ahadi
zile zile kila mwaka
11. Tusidanganyike, CCM hawana jipya
12. Chagueni UKAWA wenye dira ya
kubadili maisha ya wananchi.
13. Mimi ninauchukia umaskini na
mimesimamia maendeleo kwa
vitendo. Nilipokuwa Waziri Mkuu
nilijaribu kubadili hali hii.
Nilisimamia ujenzi wa shule za kata,
Chuo Kikuu cha Dodoma.
Nilihakikisha mikataba mibovu ya
maji inavunjwa na sasa wananchi wa
kanda ya ziwa wanapata maji safi.
Ndugu watanzania
14. CCM wanauliza tuna mpango gani wa
kumaliza umaskini. Sisi hatuahidi
tu. Tutatenda.
15. Ilani yetu ni dira ya kuondoa
umaskini kwa mikakati sahihi na
siyo nadharia.
16. Mkakati wa kuondoa umaskini si wa
sekta kwa sekta bali wa sekta zote
kwa pamoja. Ni ujumla wa utendaji
na utekelezaji wa sera za kila sekta
utakao leta maendeleo.
17. Mkakati wangu na UKAWA wa
kuondoa umaskini utakuwa na nguzo
tano:-
1. Kupunguza matumizi ya
serikali na mashirika yake na
kuimarisha utendaji na
uwajibikaji.
2. Kukuza pato la serikali kwa
kudhibiti ukwepaji na
misamaha ya kodi holela na
kuhakikisha nchi inawekeza
katika sekta muhimu na
inapata gawio halisia kutoka
wawekezaji
3. Kukuza uchumi kwa sera na
sheria endelevu ikiwa ni
pamoja na kukuza biashara na
uwekezaji hasa katika sekta za
madini, kilimo, viwanda,
ufugaji na uvuvi na kuondoa
kodi kwa wanyonge.
4. Kuimarisha huduma za umma
kama elimu, afya, maji na
makazi, na mazingira
5. Kuimarisha utawala bora na
mfumo wa haki na sheria chini
ya Katiba ya Wananchi.
18. Chini ya misingi hii na ili
kufanikisha mkakati wa kuondoa
umaskini, serikali yangu itafanya
yafuatayo:-
ELIMU BORA KWA KILA MTANZANIA
Nimelisema hili huko nyuma. Nalisema
tena leo. Elimu kwanza, Elimu kwanza,
Elimu kwanza.
Kwa hiyo mkakati wetu wa msingi
utakuwa kutoa Elimu itatayogharamiwa
na serikali kwa kila Mtanzania kutoka
elimu ya msingi hadi Chuo Kikuu na
pia:-
1. Kuimarisha elimu ya teknolojia,
ustadi na ufundi inayojenga uwezo
wa kujiajiri na ushindani katika soko
la ajira.
2. Ujenzi na uimarishaji wa
miundombinu ya elimu ikiwa ni
pamoja na shule za Kata.
3. Kusimamia ubora wa viwango vya
elimu kote nchini.
4. Kuimarisha taaluma na mitaala
katika mashule.
5. Kuondoa utoro darasani, na
kuboresha afya za wanafunzi.
6. Kuboresha maslahi na vitendea kazi
kwa walimu ikiwa ni pamoja na
nyumba, posho ya kufundishia,
usafiri na zana za teknolojia.
7. Kufuta michango ya maabara ya
shule za kata
AFYA
1. Afya na tiba ya kila Mtanzania
itagharamiwa kupitia bima za
gharama nafuu na mifuko ya hifadhi
ya jamii
2. Tutaimarisha afya ya msingi pamoja
na kinga kupunguza gharama za
tiba.
3. Serikali itahakikisha kuna uwiano na
upatikanaji wa watumishi wa afya
katika kada mbalimbali ili kuleta tija
na huduma stahiki.
4. Itaimarisha miundombinu ya afya
pamoja na kujenga hospitali za
kisasa ili kusogeza huduma za afya
karibu na jamii na pia kuepukana na
tiba za nje ya nchi.
5. Tutarejea kwa lengo la kuboresha
maslahi na vitendea kazi katika
sekta ya Afya ikiwa ni pamoja na
nyumba na usafiri.
6. Tutathibiti ongezeko la gharama za
huduma za afya bila kuathiri
uendeshaji wa watoaji huduma za
afya kama vile serikali na hospitali
za sekta binafsi.
ARDHI, MAJI NA KILIMO
1. Tutaimarisha mfumo wa umiliki wa
ardhi kwa Watanzania na kudhibiti
migogoro ya ardhi hasa kati ya
wakulima na wafugaji.
2. Tutapima ardhi yote ya Tanzania na
kumilikisha vijiji na wakulima kwa
hati za serikali ili kuipa thamani.
3. Tutaleta mapinduzi ya kilimo kwa
kuimarisha elimu, ufundi na
teknolojia ya kisasa na kumkomboa
mkulima kutoka jembe la mkono.
4. Tutasimamia kilimo, ufugaji na uvuvi
wa kisasa na kuunganisha sekta hizo
na ya viwanda.
5. Kuhakikisha kuwa wananchi
wanatunza na kulinda vyanzo vya
maji.
6. Tutakuza kilimo cha umwagiliaji kwa
kuwapa wakulima elimu na mikopo
ya riba nafuu ya kuvuna maji na
kujenga miundombinu husika.
7. Tutaweka mazingira rafiki
yatakayomhakikishia kwa kila
Mtanzania kupata maji safi na
salama. Kumaliza kero za maji
nchini kutamkomboa mwanamke
kutokana na adha ya kuchota maji
kwa kichwa
8. Nitafuta kodi zote za mazao na
mifugo kwa wakulima na wafugaji.
9. Tutasimamia kilimo cha biashara
kinachozingatia maslahi ya nchi na
ya Watanzania.
10. Tutaanzisha programu maalum ya
kufufua mazao asilia ya Tanzania
hususan mkonge.
11. Tutaanzisha Benki ya Maendelo ya
Ufugaji na Uvuvi.
MIUNDOMBINU
1. Tutaboresha bandari zilizopo na
kujenga mpya kama vitega uchumi
vya Taifa ili kurejesha biashara
tulizopoteza kwa bandari za nchi
jirani.
2. Tutajenga barabara nchini kwa
kuzingatia ubora hasa zile za vijijini.
3. Tutajenga reli ya kati kwa viwango
vya kisasa
4. Tutajenga shirika la Ndege la Taifa
linalojiendesha kwa misingi ya faida.
5. Tutajenga miundombinu ya kisasa na
kuondosha misongamano ya magari
hasa katika majiji ya Dar es salaam,
Mwanza, Mbeya na Arusha
6. Tutaimarisha uzalishaji na
usambazaji wa umeme vijijini ili
kufikia zaidi ya asili mia sabini na
tano ya Watanzania
VIWANDA
1. Tutaimarisha sekta ya viwanda kuwa
mhimili wa uchumi kwa uzalishaji
wa bidhaa na ajira endelevu
2. Tutajenga viwanda vipya vya
kusindika mazao ya kilimo, uvuvi na
ufugaji.
3. Tutahakikisha kuwa ndani ya miaka
mitano mali ghafi zote za Tanzania
zinasindikwa kabla ya kusafirishwa
nje ili kuongeza mapato na ajira ya
mamilioni ya vijana.
4. Tutaanzisha Benki ya Ukuzaji wa
Viwanda
UCHUMI
1. Tutabadili mfumo wa Uchumi wa
nchi ili kuhakikisha kuwa mfumo wa
uchumi wa Tanzania unakuwa ni wa
soko-kijamii ambapo nguvu za soko
zitatumikia jamii kwa serikali
kuweka uwiano wa mapato
unaohakikisha huduma za kijamii
zinapatikana kwa ufanisi.
2. Tutalinda sekta binafsi na bidhaa za
ndani kwa kuwapa Watanzania
upendeleo wa maksudi kwa kipindi
cha mpito ili waimarike na waweze
kuhimili ushindani. Tutawapa
wafanyabiashara wetu upendeleo
katika manunuzi ya serikali na
kuwajengea mazingira mazuri ya
biashara na kodi endelevu.
3. Tutawawezesha Watanzania kupata
mitaji ya biashara kwa masharti
nafuu kabisa.
4. Tutavutia uwekezaji na wawekezaji
wenye tija. Kuweka udhibiti wa
wahamiaji wasioleta tija wala
maslahi kwa Taifa.
5. Tutaimarisha sera ya ubia baina ya
Serikali na Sekta binafsi kwenye
maeneo muhimu ya kiuchumi na
kibiashara. Pia, kuwawezesha
Watanzania kuwekeza kwa njia ya
ubia na wawekezaji wenye mitaji
mikubwa bila kujali wanapotoka.
6. Tutaimarisha usimamizi kwa
kubadilisha mfumo wa Vyama vya
Ushirika nchini ili utokane na
uendeshwe na wakulima wenyewe
ikiwa na pamoja na kuwawezesha
kuboresha makazi kwa mpango wa
kushirikiana kujenga nyumba bora
7. Tutaanzisha na kuwezesha
uanzishaji wa viwanda vidogovidogo
vinavyotoa ajira kwa wingi kwa
kuvihusisha na vyuo vya ufundi na
benki maalum kwa lengo hilo.
AJIRA
1. Tutasimamia swala la ajira hasa kwa
vijana kwa kukuza elimu ya ufundi
ili waweze kujiajiri
2. Tutazipa kipaumbele sekta
zinazozalisha ajira kwa wingi hasa
za viwanda, kilimo, ufugaji, uvuvi na
utalii na kuzipa unafuu wa kodi ili
zikue kwa haraka.
3. Tutawapa wawekezaji wakubwa
katika sekta hizi upendeleo maalum
na viwango vya kodi nafuu.
NISHATI NA MADINI
1. Serikali itashiriki kikamilifu katika
uzalishaji wa nishati
2. Itatengeneza mazingara mazuri ya
kisera yatakayovutia na kuwezesha
ushiriki wa Watanzania na ubia kati
yao na wageni.
3. Serikali yangu itaupa uzalishaji
mkubwa wa umeme wa maji
kipaumbele namba moja, umeme wa
makaa ya mawe kipaumbele namba
mbili, umeme wa gesi asilia
kipaumbele namba tatu na umeme
wa urana kipaumbele namba nne.
4. Serikali itatoa vipaumbele muhimu
kwenye usambazaji wa huduma
kubwa ya umeme sehemu za
uzalishaji uliyolenga masoko ya
ndani, ya nchi jirani na ya nchi za
kigeni.
5. Itapitia upya mikataba yote mikubwa
ya nishati na madini ili kubaini iliyo
mibovu na kuifanyia maboresho.
6. Serikali yangu itatumia sehemu ya
hisa zake kwenye raslimali kubwa ya
gesi asilia iliyopatikana hapa nchini
kama rehani kwenye kujichukulia
mikopo kwa ajili ya ujenzi wa
miundo mbinu ya mabomba ya gesi.
7. Serikali itatoza kodi na ada ndogo
zaidi kwa wazawa wenye ubia kati
yao na wageni kuliko zitakazotozwa
kwa wageni wasiowekeza kwa
kushirikisha wazawa.
8. Serikali itasitisha utoaji wa
misamaha ya kodi isiyo lazima
kwenye sekta ya madini, na badala
yake itawekeza kwenye kuongeza
thamani ya raslimali zake za madini.
9. Tutakuza nishati mbadala
kutamkomboa mwanamke kutokana
na adha ya kukata kuni.
MALIASILI NA UTALII
1. Tutasimamia uvunaji na matumizi ya
rasilimali za Taifa kwa manufaa ya
kila Mtanzania wa kizazi hiki na
kijacho
2. Tutapiga vita ujangiri na kuimarisha
utunzanji wa hifadhi za taifa na
mazingira
3. Tutachochea ujenzi wa miundombinu
ya utalii nchini ikiwa ni pamoja na
ujenzi wa mahoteli na kuimarisha
mafunzo
4. Tutaongeza idadi ya watalii kufikia
milion mbili ifikapo 2020.
UTAWALA BORA, ULINZI WA NCHI NA
USALAMA WA RAIA
1. Tutasimamia Katiba mpya inayolinda
haki za msingi za wananchi na
kuweka bayana mipaka ya madaraka
ya serikali na viongozi, Bunge na
Mahakama.
2. Tutasimamia haki za raia na
kuangalia upya sheria kandamizi ili
wananchi kama Masheik wa Zanzibar
hawasoti jela kwa sababu za kisiasa.
3. Tutaimarisha mafunzo ya vyombo ya
Polisi hasa wapelelezi na waongoza
mashtaka ili wapate uwezo wa
kusimamia utoaji wa haki.
4. Tutavipa vyombo vyote vya ulinzi na
usalama nyenzo na kuboresha
mazingira yao ya kazi na maslahi
UZALENDO, UTENDAJI NA UWAJIBIKAJI
1. Tutajenga uzalendo ili kila
Mtanzania aweze kutathmini
mchango wake kwa taifa kila siku
2. Tutaimarisha nidhamu, utendaji na
uwajibikaji katika Sekta ya Umma
3. Tutaimarisha mchango wa Wataalam
wetu, wanawake na vijana katika
kusimamia uchumi na kuwajengea
mazingira stahiki ya kazi pamoja na
mafao.
4. Tutapiga vita rushwa na ubadhirifu
katika sekta ya Umma na binafsi
5. Tutadhibiti na kupunguza matumizi
ya serikali ikiwa ni pamoja na kufuta
safari za watumishi serikalini
zisizokuwa muhimu pamoja na zile
za Rais na kupiga marufuku
matumizi ya mashangingi serikalini.
6. Tutadhibiti deni la Taifa kwa kuanza
na ukaguzi wa madeni ya serikali ili
kuhakiki jinsi yalivyotumika
7. Tutaimarisha uwazi na kuondoa usiri
katika shughuli za serikali na
kuweka bayana mikataba yote ya
nchi ikiwa ni pamoja na ile ya
mafuta, madini na gesi asilia
KUKUZA PATO LA SERIKALI
1. Tutadhibiti mapato kutokana na
raslimali kwa kupitia upya viwango
vya mirabaha kutokana na madini na
gesi asilia ili kuhakikisha kuwa
Tanzania inapata gawio stahiki.
2. Serikali itaanzisha Wizara maalum
itakayosimamia nishati ya gesi na
mafuta.
3. Tutaimarisha ofisi ya Msajili wa
Hazina ili kusimamia vema
uwekezaji wa Serikali katika
mashirika na mapato yake.
4. Tutahakikisha kuwa mashirika ya
umma yanaendeshwa kwa misingi ya
faida na uadilifu.
5. Tutadhibiti ukwepaji kodi za ushuru
wa forodha na kupiga marufuku
misamaha ya kodi holela ili kuokoa
mabilioni ya fedha yanayopotea kila
wiki.
6. Sambamba na hilo tutarahisisha
utaratibu wa kulipa kodi ili kuondoa
kero na mazingira ya rushwa. Kwa
kudhibiti makusanyo ya kodi
tutakusanya fedha za kugharimia
huduma za msingi kama afya na
elimu kikamilifu.
KUIMARISHA MUUNGANO
1. Tutaimarisha umoja, usalama na
udugu wa Watanzania na Muungano
kwa misingi ya haki na usawa
WANAWAKE, WATOTO NA WAZEE
1. Wanawake watapewa fursa na haki
sawa katika elimu na uchumi ili
waweze bila kuwezeshwa.
2. Tutahakikisha wazazi wanapata fursa
ya kuwa walezi na wafanyakazi kwa
kuongeza urefu wa likizo ya uzazi
3. Tutaimarisha elimu ya watoto hasa
wasichana na kukuza fursa zao na
kukomesha ndoa za watoto wadogo.
4. Tutaongeza uwakilishi wa akina
mama katika ngazi zote serikalini na
mashirika yake kufikia asili mia
hamsini ifikapo 2020.
5. Wazee na wasiojiweza watapewa
posho ya kujikimu inayokidhi
mahitaji ya msingi
itakayowawezesha kuishi kwa
heshima na kulinda utu wao ndani
ya familia na jamii zao.
SANAA, UTAMADUNI
NA MICHEZO
1. Tutaendeleza na kuwezesha vipaji
vya sanaa na michezo
2. Tutarudisha viwanja vya michezo
vilivyovamiwa
3. Tutafuta kodi zote za vifaa vya
michezo.
4. Tutadhibiti viwango na maadili ya
bidhaa za nje zinazoingizwa nchini
na kuzitoza kodi halisia
5. Tutajenga taasisi na vyuo vya
kukuza michezo ili kuhakikisha kuwa
ndani ya miaka mitano Tanzania
inashiriki kwa ushindi katika
mashindano ya kimataifa ya soka na
riadha
6. Tutalinda Hakimiliki za sanaa nchini
7. Tutafuta kodi za sanaa kwa wasanii
chipukizi ili kuwapa muda kwa
kujijenga.
SERA YA MAMBO YA NJE YENYE TIJA
KWA TAIFA
1. Tutakuza ushirikiano wa Kimataifa
wenye tija na Ujirani mwema.
2. Tutatetea haki za binadamu, usawa
wa nchi na kuimarisha ushiriki wa
Tanzania katika diplomasia ya
kimataifa.
3. Tutakuza umoja na ushirikiano wa
Umoja wa Afrika, Jumuia ya Afrika
Mashariki, SADC na Umoja wa
Mataifa.
4. Tutaimarisha Umoja wa Mataifa
ikiwa ni pamoja na kudai mabadiliko
ya mfumo ili kuleta usawa wa nchi
shiriki.
Ndugu Watanzania
Naomba nimalizie kwa kusema yafuatayo
1. Natambua kuwa uongozi ni
dhamana. Mkinichagua nitaienzi
dhamana hiyo kwa utendaji
uliotukuka.
2. Nawaahidi Watanzania kuwa kwa
uwezo, akili, uzoefu na nguvu zangu
zote nitawatumikia. Nawaomba nanyi
mniahidi jasho lenu na uwezo wenu
wote ili kwa pamoja tuvuke.
Tutajikomboa toka utawala wa CCM
unaodumaza uchumi na maendeleo.
Tutaanza safari ya uhakika kuondoa
umaskini.
3. Mabadiliko pia ni kuthamini utu na
kukataa hadaa ya hongo ili kuuza
haki yako ya kuchagua. Msikubali
rubuni za uchaguzi kwa kupewa pesa
au vitu. Rushwa ya uchaguzi ndiyo
sera ya CCM. Ukikubali basi umeuza
pia haki na sauti yako ya
kuwalalamikia walio madarakani.
Imetosha. Tukatae. Tulinde utu na
haki zetu. Tuchague mabadiliko.
4. Mabadiliko ni fikra. Ni kufikiri na
kutenda tofauti. Hatuwezi kuendelea
kufikiri na kutenda kama kwamba
hatuna dharura ya maendeleo.
Kwanza tuanze kwa kufanya
mabadiliko na tujiamini kuwa sisi
kama Taifa tunaweza. Tunaweza
kujitegemea na kuleta maendeleo
yetu wenyewe bila kutegemea
wafadhili. Hii si ndoto. Nchi nyingi
zimefanikiwa kuondoa umaskini
katika kizazi kimoja. Tujifunze
kutoka kwao.
5. Tuwe taifa linalotumia raslimali zake
kujiendeleza na siyo kuwanufaisha
wageni na kuwafanya Watanzania
watwana katika nchi yao. Inabidi
tuache kuwa taifa ombaomba.
Tuache kuukubali na kuvaa umaskini
kama joho la fahari.
6. Mabadiliko ya kweli hayawezi
kuletwa na CCM. Tusitegemee kuwa
leo wana jipya. Ndiyo maana ahadi
walizotoa miaka thelathini iliyopita
ndizo wametoa juzi. Tukatae hadaa.
Miaka hamsini ya CCM imetosha.
7. Tunaamani kwamba tutashinda kwa
sababu Watanzania mpo nyuma yetu.
Watanzania mmeamua kuleta
mabadiliko. Kura yako ndiyo
itakayokuwa mkombozi wako.
Hakikisha unapiga na kuilinda kura
yako. Wakati wa mabadiliko ni sasa.
Mungu ibariki Tanzania. Asanteni sana
0 comments :
Post a Comment