JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA COMMUNICATIONS REGULATORY ISO 9001:2008 CERTIFIED
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MFUMO WA RAJISI YA NAMBA ZA UTAMBULISHO WA SIMU ZA KIGANJANI (CENTRAL EQUIPMENT IDENTIFICATION REGISTER (CEIR)
UTANGULIZI:
Vifaa vya mawasiliano vya mkononi – hususan simu za kiganjani na vifaa
vya mawasiliano vya kiganjani (tablets) – vina namba maalum
inayovitambulisha. Namba hiyo inajulikana kama IMEI ambacho ni kifupi
cha International Mobile Equipment Identity.
Kifungu cha 84 cha
Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) ya 2010 kinataka
kuwepo kwa mfumo wa rajisi ya namba za utambulisho wa vifaa vya
mawasiliano vya mkononi. Rajisi hii inajulikana kwa kiingereza kama
Central Equipment Identification Register, kwa kifupi CEIR. Sheria
inataka rajisi hiyo ihifadhiwe na kuendeshwa na Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania.
Aidha Kanuni za mwaka 2011 za EPOCA kuhusu mfumo wa rajisi
ya namba za utambulisho wa vifaa vya mawasiliano vya mkononi inawataka
watoa huduma wa mawasiliano yanayotumia vifaa vya mkononi kuweka mfumo
wa kudumu wa kumbukumbu za namba tambulishi (Equipment Identity Register
– EIR) za vifaa vya mkononi vinavyotumika kwenye mitandao yao.
Mfumo huu wa kielektroniki ambao utahifadhi kumbukumbu za namba
tambulishi za vifaa vya mawasiliano vya mkononi una lengo la kufuatilia
namba tambulishi za vifaa vinavyoibiwa, kuharibika, kupotea au ambavyo
havikidhi viwango vya matumizi katika soko la mawasiliano. Vifaa vyote
vya mawasiliano vya mkononi ambavyo vimeibiwa, vimeharibika, kupotea au
visivyokidhi viwango vya matumizi katika soko la mawasiliano havitaweza
kufanya kazi kwenye mitandao ya mawasiliano kutumia vifaa vya mkononi.
UFAFANUZI
Taarifa kwenye mfumo huu wa rajisi zitakuwa na aina tatu za kumbukumbu;
ambazo ni orodha ya namba tambulishi ambazo vifaa vyake vinaruhusiwa,
orodha ya namba tambulishi ambazo zimetolewa taarifa kuwa zimefungiwa na
namba tambulishi ambazo zimefungiwa kwa muda au kuruhusiwa kwa muda.
Orodha Nyeupe:
Orodha ya vifaa vya mkononi vya mawasiliano vinavyoruhusiwa kutumika katika mitandao ya huduma za simu za kiganjani
Orodha Nyeusi:
Orodha hii ni ya namba tambulishi ambazo zimefungiwa na mtoa huduma
kwenye mfumo wao wa EIR na kutumwa kwenye mfumo wa CEIR kwa ajili ya
kufungiwa ili zisitumike kwenye mitandao mingine ya simu za kiganjani
kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa na kukubaliwa miongoni mwa watoa
huduma. Simu zote za mkononi zilizoibiwa au kupotea zitafungiwa ndani ya
saa 24 ili zisitumike kwenye mtandao wowote wa simu za mkononi
Tanzania.
Ikitokea simu ya mtumiaji ikafungiwa kinamosa, anatakiwa
kutoa taarifa mara moja kwa mtoa huduma wako kwa ajili ya kuifungua.
Watoa huduma wanatakiwa wafungulie, ndani ya saa 24, simu zote
zilizofungwa kimakosa.
Orodha ya kijivu:
Orodha hii ni ya namba tambulishi ambazo zimefungiwa au kufunguliwa kwa muda kwa lengo la kuanzisha mchakato wa kuzifuatilia.
FAIDA ZA MFUMO WA RAJISI YA NAMBA TAMBULISHI
Mfumo huu wa rajisi una faida zifuatazo:
1. Kuthibiti wizi wa simu. Iwapo mtu atapoteza au ameibiwa simu ya
kiganjani na akatoa taarifa kwa mtoa huduma, simu hiyo itafungiwa
isiweze kutumika kwenye mtandao mwingine wowote wa simu za kiganjani.
Mteja anaponunua simu ni lazima adai risiti halali na halisi na pia
garantiii ya angalau miezi 12. Mteja anatakiwa aihifadhi risiti hiyo
angalau kwa miezi mitatu. Baada ya hapo, iwapo simu imekuwa inatumika,
taarifa za matumizi zinaweza kutumika kama uthibitisho mbadala wa milki
ya simu husika.
2. Kuhimiza utii wa sheria: Kifungu cha 128 cha
EPOCA kinamtaka mtumiaji wa simu kutoa taarifa ya kupotea au kuibiwa kwa
simu au laini ya simu. Kifungu cha 134 kinayataka makampuni ya simu
kutokutoa huduma kwa simu ambayo imefungiwa kama ilivyoelezwa hapo juu.
Mara tu mteja anapopoteza simu yake ya kiganjani anatakiwa kutoa taarifa
kwa kituo cha Polisi cha karibu ambapo atapewa namba ya kumbukumbu ya
taarifa ya tukio, maarufu kama RB. Anatakiwa aende kwa mtoa huduma kutoa
taarifa ya tukio akiwa na hiyo RB na uthibitisho wa umilki wa simu
iliyopotea ( risiti aliyopewa wakati wa kununua iwapo itakuwepo). Mtoa
huduma kwanza atahakiki umilki wa simu iliyopotea au kuibiwa na
atampatia mteja namba ya kumbukumbu kwamba simu hiyo imefungiwa
isutumike kwenye mitandao ya simu na hatimaye ataifungia simu hiyo ndani
ya saa 24.
3. Kujenga misingi ya matumizi ya simu halisi, zisizo
bandia. Mtumiaji ataweza kutambua iwapo simu aliyo nayo inakidhi
viwango, ni halisi na sio bandia.
KUTAMBUA NAMBA TAMBULISHI
Ili kutambua namba tambulishi ya simu ya kiganjani au vifaa vya
mawasiliano ya kiganjani, mtumiaji anatakiwa aandike tarakimu *#06# kwa
kutumia kifaa chake. Baada ya kufanya hivyo, kutaonekana namba ndefu.
Mtumiaji anatakiwa kuandika namba hiyo kama ilivyoonekana kwenye kifaa
chakena kuihifadhi katika hali ya usalama kwa ajili ya rejea ya baadae.
Baada ya hapo mtumiaji atume ujumbe mfupi wenye hiyo namba tambulishi
kwenda namba 15090. Atapokea meseji itakayomjulisha kuhusu hali halisi
ya simu yake ya kiganjani. Mtumiaji atapokea ujumbe kuhusu uhalisia wa
simu yake. Majibu yatakayokuja yatasomeka: Kama IMEI haioani na aina ya
simu yako, wasiliana na aliyekuuzia. Usipoweza,ibadilishe kabla ya Juni
2016 kwani simu hiyo inaweza kuwa BANDIA.
Watumiaji wanaweza pia kuhakiki uhalisia wa simu zao za kiganjani kupitia tovuti ya Mamlaka ya Mawasiliano kwa kuandika http://www.tcra.go.tz/index.php/imei-code-verification
HATUA ZA KUCHUKUA IWAPO SIMU ITAONEKANA HAIKIDHI VIWANGO, SI HALISI NA NI BANDIA
Mtu yeyote ambaye atatambua kwamba simu yake ya kiganjani si halisi,ni
bandia na haikidhi viwango atapewa muda wa kuendelea kutumia simu hiyo.
Baada ya muda huo kumalizika, simu hiyo itaingizwa katika orodha nyeusi
na kufungiwa isitumike kwenye mitandao mingine yoyoye ya simu za
kiganjani.
Watumiaji wote wenye simu za kiganjani ambazo namba
tambulishi zao zinaonyesha kwamba simu hizo si halisi, ni feki na
hazikidhi viwango watagharamia ununuzi wa simu nyingine. Watumiaji wote
ambao namba tambulishi za simu zao zinaonyesha kwamba vifaa hivyo si
halisi, ni feki na havikidhi viwango watatakiwa kubadilisha simu hizo na
kupata zinazokidhi viwango na halisi katika muda wa miezi sita kuanzia
siku ya uzinduzi wa mfumo wa rajisi ya namba za utambulisho wa simu za
kiganjani.
Ni vyema ifahamike kwamba simu zote za kiganjani na vifaa
vya mawasiliano vya kiganjani (tablets) ambazo zitakuwa na namba
tambulishi bandia zitafungiwa kuanzia 16 Juni 2016.
HITIMISHO
Mfumo wa Rajisi ya Namba za Utambulisho wa vifaa vya mawasiliano vya
mkononi una lengo la kuwahakikishia watumiaji usalama wakati wanapotumia
vifaa hivyo vya mawasiliano, vikiwemo simu za kiganjani na vifaa vya
mawasiliano vya kiganjani (tablets). Uanzishwaji wake ni sehemu ya
kutekeleza matakwa ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya
2010. Ni vyema watumiaji wakazingatia maelekezo kuhusu utaratibu wa
kuhakiki namba tambulishi, kutoa taarifa wanapopoteza au kuibiwa simu.
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
18 December 2015
-
Blogger Comment
-
Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments :
Post a Comment