TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Kama ambavyo imeripotiwa kwenye
vyombo vya habari na njia zingine za upashanaji habari tangu jana kuwa
Mbunge wa Jimbo la Ubungo kwa tiketi ya CHADEMA, Ndugu Saed Kubenea
aliwekwa chini ya ulinzi na kuamriwa kwenda kituo cha polisi kwa amri ya
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda ambaye inadaiwa hakutaka
mbunge huyo azungumze na wananchi ambao ni Wafanyakazi wa Kiwanda cha
Tanzania Took Garment, waliokuwa wamemuita mbunge huyo kwa ajili ya
kumweleza matatizo wanayokumbana nayo kazini hapo, ikiwa ni pamoja na
ujira kidogo na mazingira magumu ya kazi.
Aidha akitambua kuwa
alichofanya matumizi mabaya ya dhamana ya uongozi, hivyo akakusudia
kuficha umma usijue uovu huo, katika tukio hilo Makonda aliwaagiza
polisi wakamate kamera za waandishi wa habari waliokuwa katika eneo hilo
wakitimiza wajibu wao wa kikazi na kitaaluma kwa jamii.
Katika hatua ya sasa, tunaomba kusema ifuatavyo;
1. Tukitambua kuwa mamlaka ya DC kuamuru watu kukamatwa yamefafanuliwa
kisheria na kuwekewa mipaka yake ambayo Makonda amedhihirisha kuivuka
katika nyakati tofauti sasa, Mkuu huyo wa wilaya hana mamlaka ya
kisheria wala ya kisiasa kuhalalisha amri aliyoitoa ya kumkamata mbunge,
tena aliyekuwa anatekeleza wajibu wake, tunamtaka DC Makonda amwachie
Ndugu Kubenea mara moja huku tukitoa wito kwa mamlaka zilizomteua
kumwangalia kwa makini kama bado anazo sifa za kuwa kiongozi wa ngazi
hiyo.
2. Kwa kuwa amri hiyo si halali kwa sababu haina msingi
wowote wa kisheria, tunatoa wito kwa Jeshi la Polisi kumuachia Ndugu
Kubenea ili aendelee na uhuru wake huku akitekeleza wajibu wake wa
kuwawakilisha wananchi wa Ubungo badala ya kumsumbua kwa mambo
yasiyokuwa ya msingi.
3. Halikadhalika, Jeshi hilo liwarudishie
waandishi wa habari vifaa vyao vya kazi vikiwa katika hali salama na
bila athari yoyote ama ya vifaa vyenyewe au materials yaliyoko ndani
yake.
4. Tunalitaka Jeshi la Polisi kutoa kauli ya
kuwahakikishia usalama waandishi wa habari na vifaa vyao kila
wanapotimiza wajibu wao kwenye matukio yanayomhusisha Makonda kwa sababu
tayari ushahidi unaonesha anaweza kuwa tishio kwao binafsi na vitendea
kazi vyao hususan pia wanapokuwepo polisi.
5. Kwa kitendo cha DC
Makonda kuamuru kiongozi wa wananchi akamatwe bila kuwepo kosa lolote la
kisheria, CHADEMA tutachukua hatua za kisheria dhidi ya DC huyo ili
liwe fundisho kwake mwenyewe, wakuu wa wilaya wengine na utawala mzima
wa Serikali ya CCM chini ya Rais John Magufuli, ili watambue kuwa suala
la kuongoza nchi kwa kuzingatia Haki, Katiba, Sheria na taratibu si
suala la kupenda bali ni lazima kuzingatiwa kwa ajili ya amani na
utulivu wa kweli.
Tutachukua hatua hizo huku tayari kukiwa na
kumbukumbu za Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBU) ambayo
hivi karibuni ilimuonya DC Makonda na wakuu wa wilaya wengine na wakuu
wa mikoa ambao wameanza tabia ya kuendesha nchi kwa amri ambazo hazina
uhalali wowote zikiwa nje ya mamlaka yao ya kisheria kufanya hivyo.
Tuliamini angalizo hilo la THUB ambacho ni chombo huru cha serikali,
lingeweza kuwa mwongozo sahihi kwa viongozi wa serikali na kwamba kosa
la awali la Makonda kuwaweka mahabusu watumishi wa Wilaya ya Kinondoni
walioko chini yake lingechukuliwa kama fundisho kwake, lakini bahati
mbaya watawala wanaweka nta masikioni linapofika suala la haki za
binadamu na uongozi bora.
Imetolewa leo Jumanne, Nov. 15, 2015 na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA
Home
/
Uncategories
/
TAMKO LA CHADEMA BAADA YA MKUU WA WILAYA KUTUMIA MAMLAKA YAKE VIBAYA DHIDI YA KUBENEA NA VYOMBO VYA HABARI
-
Blogger Comment
-
Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments :
Post a Comment