Salma Said
Viongozi wa kisiasa wanaokutana kwa ajili
ya mazungumzo ya kuutatua mkwamo wa kisiasa Zanzibar wamekutana tena
jana kwa mara ya sita Ikulu Mjini Zanzibar. Mazungumzo hayo
yanawajumuisha wagombea urais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein na
Maalim Seif Sharif Hamad pamoja na marais wastaafu akiwemo Mzee Ali
Hassan Mwinyi, Dk Salmin Amour Juma, Dk Amani Abeid Karume na Balozi
Seif Ali Iddi.
Mazungumzo hayo ambayo yalianza Novemba 9
mwaka huu yamekuja kufuatia mgogoro wa kisiasa ambao umetokana na
uchaguzi mkuu uliofanyika Octoba 25 mwaka huu kugubikwa na giza nene
kutokanana na kufutwa kwa uchaguzi mkuu siku tatu baada ya wananchi
kupiga kura zao na baadhi ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa.
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar
(ZEC) Jecha Salum Jecha mnamo Octoba 28 alitangaza kuufuta uchaguzi mkuu
wote wa Zanzibar kwa madai ya kuwepo kasoro zilizojitokeza katika
uchaguzi huo jambo mbalo limepingwa vikali na viongozi wa Chama Cha
Wananchi (CUF) pamoja na waangalizi wa uchaguzi wa ndani na nje ya nchi
ambao walitoa tathmini zao za kufanyika uchaguzi huru, uwazi na haki.
Hata wanasheria kupitia Jumuiya ya
Wanasheria ya Zanzibar (ZLS) walipinga hatua ya Mwenyekiti wa tume
wakisema hana mamlaka ya kisheria ya kufuta uchaguzi kwa mujibu wa
sharia No 11 ya Uchaguzi ya Zanzibar ya mwaka 1984.
Hadi sasa hakuna kiongozi yeyote
anayeshiriki mazungumzo hayo ambaye yupo tayari kuzungumzia nini khsa
wanachojadiliana na mpaka lini watatoa taarifa kwa umma.
Lakini taarifa ndani ya kikao hicho
zinasema kwamba kikao hicho tokea kuanza kwake licha ya changamoto za
hapa na pale mazungumzo yanakwenda vizuri huku kila mmoja akiweka
maslahi ya taifa mbele badala ya kuweka mbele mtazamo wa chama chake.
Viongozi wote wanaokutana ni kutoka Chama
Cha Mapinduzi isipokuwa Maalim Seif ambaye ndiye kutoka chama cha
upinzani cha CUF lakini licha ya kuwepo peke yake amekuwa akielewana
vyema na wenzake kwa kuweka maslahi ya taifa mbele huku ‘spirit’ ya
mazungumzo ikiwa imewekwa mbele kwa kuwa Dk Amani Karume naye ni
mshirika wa karibu wa Maalim Seif na ndiye aliyeongoza mazungumzo ya
kutafuta Mwafaka wa Zanzibar katika kipindi kilichopita cha uongozi
wake. Mazungumzo yao yalihitimishwa kwa Maridhiano yalioidhinishwa rasmi
na wananchi kupitia kura ya maoni kabla ya uchaguzi wa 2010.
Kikao hicho ambacho tokea kilipoanza
Novemba kimeendelea na mazungumzo vizuri na ilipofika Novemba 17 Dk
Shein aliondoka na kwenda kumuunga mkono Rais wa Tanzania Dk John
Magufuli katika kuzindua Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo
lilizinduliwa Novemba 20 uzinduzi ambao umefuatiwa na kuzomewa kwa Dk
Shein na wapinzani wakisema sio Rais halali wa Zanzibar kwa kuwa muda wa
kuwepo madarakani imemalizika.
Wiki moja baadae viongozi hao walikutana
tena na kurejea pale walipoishia na kila upande kuwasilisha kile
walichokubaliana katika kikao kilichopita ambapo walipeana kazi za
kufanya na kuziwasilisha katika kikao kilichofuata ambapo baadhi ya
maamuzi yamefikiwa pasi na kipingamizi chochote..
Kwa upande wa vyama vya siasa ambavyo
viongozi wao wanashiriki mazungumzo hayo kutoka CCM na CUF nao hawakuwa
tayari kuzungumza juu ya kinachoendelea huko Ikulu kwa madai kwamba
mazungumzo hayo ni ya viongozi wa juu na hayajashushwa katika ngazi ya
chama.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai
Ali Vuai alipohojiwa na Mwananchi jana alisema chama CCM kimetoa baraza
juu ya mazungumzo yanayoendelea huko Ikulu lakini kinachojadiliwa ndani
ya kikao hicho wao kama chama hawajui.
“Sisi kama chama tumeyabariki mazungumzo
yanayoendelea ya viongozi baina ya pande zote mbili kwani tunaamini
yatakuja na muelekeo mzuri wa mustakabali mwema wa nchi yetu” alisema
Vuai kwa njia ya simu.
Vuai alisema mazungumzo ya Dk Shein na
viongozi wenzake hayajafikishwa katika uongozi wa CCM na hivyo hana cha
kuongea zaidi kwa kuwa bado mazungumzo hayo ni siri lakini wanampongeza
Dk Shein kwa ujasiri wake wa kuendesha nchi katika utulivu na amani.
Vuai alisema licha ya mazungumzo lakini
taratibu za uchaguzi kufanyika tena Zanzibar ipo pale pale na wanasubiri
tume ya uchaguzi itangaze tarehe ili waweze kushiriki uchaguzi huo
kikamilifu.
“Taarifa nilonazo uchaguzi upo na
hatujapokea mabadiliko yoyote kwa hivyo sisi kama chama tunasubiri Tume
itangaze siku ya uchaguzi na tunasubiri kama wanavyosubiri vyama
vyengine watangaziwe” alisema Vuai Ali Vuai.
Kikao cha leo kinatarajiwa na wengi kuwa
ndio kitakuwa cha mwisho na baadae kusubiri maamuzi yatakayoamua
mustakabali mzima wa nchi ikiwemo kupata hatma ya uchaguzi ambao chama
cha CUF kinashikilia kuwa kina ushindi mkononi.
Kwa upande Kaimu Mkurugenzi wa Habari na
Mawasiliano wa CUF, Ismail Jussa Ladhu alisema wanazo taarifa za
kuendelea mazungumzo hayo lakini jambo la msingi ni kwamba umefika
wakati mazungumzo hayo yakamilishwe na matokeo yake yaelezwe kwa
wananchi.
“Mazungumzo haya yanahusisha viongozi
wetu na makubaliano yao ni kwamba kama ni taarifa basi watatoa wenyewe
kwa pamoja. Kwa hivyo, mimi siwezi kuzungumzia chochote kwa sasa”.
Alisema Jussa.

0 comments :
Post a Comment